Monday 21 October 2013


Si wengi wetu wanaofahamu umuhimu wa kula samaki mara kwa mara na jinsi kitoweo hiki kilivyo na umuhimu wa kipekee katika afya ya binadamu
Samaki ni kitoweo ambacho kinatajwa na hata kupendwa na wengi, binadamu au wanyama.
Kitoweo hiki kinaelezwa kuwa na mafuta yenye kiambata aina ya Omega 3 yanayomfanya binadamu kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, kutunza kumbukumbu na kuishi kwa muda mrefu.
Vyakula vyote vinavyozalishwa majini huwa na kiambata aina ya Omega 3 yenye mafuta yanayotakiwa kwa mwili wa binadamu yatokanayo na samaki, yana mbegu maalumu zinazomsaidia binadamu katika ukuaji ambazo pia ni maalumu kwa faida ya mfumo wa ubongo na neva.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito mikubwa wamekuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, akili nyingi na wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu kutokana na kutokuzeeka mapema.
Kwa upande wa Tanzania, watu waliozaliwa na kuishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito ikiwemo kisiwa kama cha Ukerewe na maeneo mengine karibu na maziwa Victoria, Nyasa, Rukwa hata visiwani Zanzibar wamebainika kuwa ni watu wenye akili nyingi na wanaishi kwa muda mrefu ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi kitakwimu.
Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma ya Ushauri Nasaha, Lishe na Afya, Counselnuth, Mary Materu anadhibitisha kuwapo na virutubisho vingi vinavyopatikana katika kitoweo hiki cha samaki iwapo wataliwa kwa wakati mwafaka mara tu baada ya kuvuliwa.
“Samaki wana kiambata aina ya Omega 3 ambayo husaidia katika ukuaji wa binadamu na kujenga ubongo wake vizuri, ndiyo maana watu wanaoishi katika maeneo yaliyozungukwa na maji mengi ‘bahari,  mito au maziwa’ ni watu wenye akili nyingi na watambuzi hata kama hajaenda shule na akienda shule hufanya vyema sana darasani kama ni mtoto, angalia watu wanaotoka ukerewe au sehemu nyinginezo,” anasema Materu.
Materu anafafanua kuwa kinamama wajawazito kwa upande wao wamekuwa wakipewa ushauri kutumia kitoweo hicho wawapo wajawazito na kuepuka nyama nyekundu ambayo hata hivyo ni muhimu kwa mama mjamzito kutumia ili kuongeza damu haraka kwa mjamzito.
“Wajawazito wanapaswa kula samaki kwa wingi ili kukuza ubongo wa mtoto, pia ni lazima wale nyama nyekundu ili kuongeza damu kwa uharaka mwilini ila tunawashauri isizidi nusu kilo kwa siku saba,” anasema Materu na kufafanua umuhimu wa Omega 3 kwa wajawazito.
“Omega 3 humsaidia mtoto kukuza ubongo, kutengeneza retina kwenye mboni ya macho na kutengeneza mfumo wa neva.
Pia, humsaidia mama kuzuia matatizo kama kifafa cha mimba na sonono baada ya kujifungua. Njia kuu ya mtoto kupata Omega 3 ni kutokana na vyakula anavyokula mama yake.
Kama mama atashindwa kupata vyakula vya kutosha vyenye Omega 3, basi mtoto atachukua ile iliyoko mwilini mwa mama ambayo mara nyingi iko kwenye ubongo wa mama.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),  Dk Cyril Masawe  anasema samaki wana umuhimu katika afya ya mama na mtoto na iwapo mama hatapata Omega 3 ya kutosha anaongeza hatari ya kupata postpartum depression, ‘mtoto mwenye uzito mdogo’, uchungu wa mapema (preterm labour), ‘mtoto kuzaliwa kabla ya muda’, au kulazimika kuzaa kwa upasuaji.
“Watoto ambao wamepata Omega 3 ya kutosha wameonyesha kuwa na umakini mkubwa na upeo mzuri kuliko watoto wengine. Pia, hukua kwa haraka zaidi kuliko yule ambaye hakupata kiambata hicho na huwa mtunzaji mzuri wa kumbukumbu. Hupunguza matatizo ya kitabia, na kwa watu wazima hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na saratani nyinginezo.
Dr Masawe anasema kuwa  Omega 3 inahitajika kwa kila binadamu ili kuendelea kuutunza ubongo na kujiepusha na magonjwa yanayotokana na kukosa madini haya.
“Ni vizuri kupata Omega 3 ya kutosha kupitia mlo wa kila siku. Wakati wa ujauzito mwanamke anashauriwa kupata angalau gramu 250 kila siku na katika kipindi cha mwisho (miezi mitatu ya mwisho) kwa sababu katika kipindi hiki mtoto hutumia asilimia 70 ya Omega 3 kujenga ubongo wake na mfumo wake wa neva.
Wataalamu hao wanaelezea vyanzo vinavyoleta madini hayo kuwa vinapatikana katika samaki na mafuta ya samaki hasa samaki wenye mafuta mengi kama vibua (mackerel), sato, salmon, sangara, dagaa, herring na jodari.

No comments:

Post a Comment