Tuesday 29 October 2013

Sera ya ujasusi yaikaba koo Marekani


Chansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Barack Obama wa Marekani

Shinikizo linazidi kuongezeka dhidi ya Ikulu ya Marekani kuelezea ukusanyaji wa taarifa za kijasusi za Marekani na kwa nini Rais Barack Obama anaonekana kutofahamu ukubwa wa tatizo hili.
Mkuu wa Shirika la Ujasusi na maafisa kadha watafika mbele ya Baraza la Wawakilishi kutoa maelezo kufuatia kadhia hiyo.

Na mwenyekiti wa kamati ya usalama ya Baraza la Seneti ametaka kupitiwa upya kwa mpango mzima wa Marekani wa ukusanyaji wa taarifa za kijasusi.
Rais Obama ameelezea hadharani nia yake ya kuchunguza shughuli za kijasusi huku kukiwa na madai ya kuzichunguza kijasusi nchi marafiki duniani.
Ujumbe wa Umoja wa Ulaya, uliopo mjini Washington umeelezea mvutano huo kuhusu ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia kuwa ni kuvunjika kwa kuaminiana kati ya Marekani na washirika wake.
Jumatatu bwana Carney, msemaji wa Rais Barack Obama, aliwaambia waandishi wa habari kuwa utawala wa Marekani unatambua umuhimu wa kujizuia zaidi katika kukusanya taarifa za kijasusi.
"Kuna mabadiliko yasiyo ya kawaida... Kwa namna tunavyotuma na kukusanya taarifa", anasema Jay Carney.
Amesema Marekani haitumii uwezo wake wa kukusanya taarifa za kiintelijensia kwa madhumuni ya kuimarisha maslahi yake ya kiuchumi, na kwamba Rais Obama amedhamiria kuhakikisha kuwa tunakusanya taarifa si tu kwa sababu tunaweza kufanya hivyo, lakini kwa sababu tunalazimika, kwa sababu tunazihitaji taarifa hizo kwa usalama wetu.
"pia tunataka kuhakikisha kuwa taarifa zetu za kiintelijensia zinafanya kazi kubwa ya kukidhi malengo yetu ya sera ya nje na usalama wa taifa, na kwamba tunapima hatari na faida ya shughuli zetu hiz. Anasema Bwana Carney.
Bwana Carney na Bwana Obama hawajazungumzia lolote kuhusu tuhuma halisi kwamba Marekani imekuwa ikifuatilia taarifa za kijasusi kutoka kwa washirika wake kimataifa, ikiwa ni pamoja na kurekodi mazungumzo ya simu ya maafisa wa nje.

No comments:

Post a Comment