Wednesday 23 October 2013

POLISI WAREJESHA VITITA VYA FEDHA ZA WACHINA MKOANI IRINGA


WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wamewateka raia wanne wa China mkoani Iringa, na kisha kuwapora fedha, zaidi ya shilingi Milioni 130 za Kitanzania, fedha za Kichina, pamoja na vifaa mbalimbali zikiwemo simu tano katika mlima wa Nyang'oro uliopo mkoani Iringa.
Akizungumzia tukio hilo kamanda wa jeshi la Polisi mkoani Iringa ACP Athmani Mungi amesema raia hao wa china wa kampuni ya SIETCO, inayojenga barabara ya Iringa- Dodoma, walikutwa na mkasa huo wakati wakirejea kutoka Iringa mjini, ambapo msako mkali wa jeshi hilo umefanikisha kupatikana kwa shilingi Milioni 80.
ACP Mungi amesema wachina hao walitekwa na kuporwa kiasi hicho cha fedha na vitu mbalimbali, mara baada ya kuchukua fedha hizo katika benki ya CRDB tawi la Iringa, na wakiwa katika gari lao aina ya Toyota yenye namba za usajili T. 335 CMX lilizuiliwa na gari kubwa aina ya Lori katika mlima wa Nyang'olo huku watu watano wenye siraha wakapora mfuko uliokuwa na fedha hizo.
Amesema majambazi hao walichukua pia simu za mkononi tano na funguo za gari la wachina na kutokomea nalo pamoja na kiasi hicho cha fedha cha shilingi Milioni 135, ambazo walikuwa wanarudi
nazo katika kambi yao ya Mtera.
"Wachina hao walikuwa wametoka kuchukua fedha hizo katika benki ya CRDB tawi la Iringa mjini bila kuwa na ulinzi wowote wa askari Polisi, na walikuwa wanazipeleka katika kambi yao iliyopo
Mtera," Alisema Mungi.
Amesema jeshi la polisi baada ya kupata taarifa hiyo walifanya oparesheni la kuwasaka majambazi hao mchana na usiku, kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji vya tarafa ya Isimani, ambapo zoezi hilo liliendelea mpaka siku ya tarehe 23 alfajiri walipowaona majambazi hao.
"Oparesheni ya kuwasaka majambazi waliofanya tukio hilo iliendelea usiku na mchana, askari polisi kwa kushirikiana na wananchi, na alfajiri ya leo majira ya saa kumi askari yaliyaona majambazi hayo na ndipo mapambano makali yalianza, huku majambazi na askari wakirushiana risasi za moto," Alisema.
Pia amesema mapambano makali yaliwachanganya majambazi hayo na kupelekea kutupa Silaha aina ya Shortgun Greener iliyokuwa imekatwa Mtutu (Kitako) ikiwa na risasi moja chemba, huku majambazi hayo yakitupa begi moja lililokutwa na shilingi Milioni 80, na lingine likiwa na Biscuit na vitu vingine vya kichina.
Mungi amesema katika oparesheni hiyo pia wamefanikiwa kumkatata jambazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuhofia kuharibu upelelezi wa kuwasaka majambazi wengine wanne waliofanikiwa kutoroka.
Mungi amesema jambazi huyo amekamatwa katika kijiji cha Itono akiwa katika gari aina ya Hiace na kukutwa na Pochi ya wachina ambayo ilikuwa na vitu vilivyoibwa kwenye eneo la tukio hilo la
utekaji.
"Vitu alivyokutwa navyo mtu tuliyemkamata ni fedha za kichina zinazofahamika kama Yuan zikiwa 97, nyingine ni fedha hizo hizo za kichina zinaitwa Jiao hizo zilikuwa tatu, leseni ya udereva mali ya mchina Gang Cheng, Leseni ya udereva ya Hua -Li-wei, Simu moja ya kichina pamoja na Vitambulisho vilivyoandikwa kwa lugha ya Kichina," Alisema Mungi.
Aidha kamanda Mungi ametoa onyo kwa majambazi kuacha mara moja uharifu kwa madai kuwa mkoa wa Iringa si salama kwa majambazi na waharifu wa aina yoyote kwani hata wanaotoka nje ya mkoa huo wakiingia kufanya uharifu hawatatoka salama, huku akiwaasa wananchi kuacha mara moja kusafiri na fedha kiasi kikubwa pasipokuwa na ulinzi wowote.
Pia Kamanda Mungi amewashukuru wananchi walioshirikiana na jeshi la polisi katika kufanikisha zoezi la kupatikana kwa fedha hizo, pamoja na baadhi ya vitu vya wachina hao.
Hata hivyo siku za hivi karibuni, gari la kampuni ya E. Awadhi, kampuni inayojihusisha na usafirishaji wa mafuta nchini Zambia na Malawi lilitekwa katika eneo la Igumbilo mjini Iringa na kisha
watekaji kutoroka na gari ambalo lilikuwa limejaza mafuta katika mataki yake, huku jeshi hilo likifanikiwa kumnasa mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo.

No comments:

Post a Comment