Monday 28 October 2013

Malinzi ambwaga Nyamlani TFF


HATIMAYE kitendawili cha uchaguzi mkuu wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) kimeteguliwa baada ya Jamal Malinzi kuibuka kidedea katika uchaguzi huo.
Malinzi aliibuka kidedea kwa kura 73 akimbwaga mpinzani wake pekee, Athuman Nyamlani (pichani) aliyepata kura 52.
Uchaguzi huo ulifanyika kwenye Ukumbi wa Waterfront, Dar es Salaam ukitanguliwa na mkutano mkuu wa TFF ulimalizika usiku wa kuamkia leo, Jumatatu saa saba na nusu.
Kuanzia asubuhi ya jana, Jumapili wapambe wa wagombea hao wawili walijazana katika ukumbi huo, huku kila upande ukijipa matumaini ya kukibeba kiti hicho.
Hata hivyo pengine kwa kusoma alama, Nyamlani aliondoka ukumbini mapema kabla hata zoezi la kuhesabu kura halijaanza hali ambayo tayari ilitoa dalili kwamba huenda mambo yalimuendea kombo.
Wakati Nyamlani akiondoka katika eneo la uchaguzi, baadhi ya wapambe wa kambi ya Malinzi walianza kuzungumza katika vikundi wakitambia ushindi wa mgombea wao.
Malinzi anatarajia kukabidhiwa rasmi ofisi na rais anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga, Jumamosi ijayo.
Katika kinyang’anyiro cha Makamu Rais, Walace Karia
aliibuka kidedea kwa kuzoa kura 67 akiwabwaga wapinzani wake, Ramadhan Nassib aliyepata kura 52 na Imani Madega aliyeambulia kura sita.
Kufanyika kwa uchaguzi huo kunamaliza fitina za wiki kadhaa zilizotawala medani ya soka nchini hususan katika nafasi ya mwenyekiti ambayo ndiyo iliyokuwa na mvuto wa kipekee miongoni mwa wadau wa soka nchini.
Uchaguzi huo unakuwa umeingiza sura mpya ambazo zitaliongoza shirikisho hilo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Vipaumbele vya Malinzi alivyovinadi katika kampeni zake ni pamoja na kukuza vipaji, kuboresha viwanja kwa kuanzisha kampuni tanzu itakayoingia mkataba na wamiliki wa viwanja ambao ni Halmashauri mbalimbali nchini na Chama cha Mapinduzi, kuwaendeleza waamuzi na makocha kimafunzo ndani na nje ya nchi.
“Nikifanikiwa nitaanza kwa kupitia mikataba yote ya wafanyakazi ukianza wa Katibu Mkuu, naamini wafanyakazi wote TFF wana mikataba, nitaangalia namna ya kuwaboreshea mishahara na kuwapa motisha, na nitaipitia mikataba ya wadhamini, kuna kampuni zinatangazwa kuanzia ngazi za wilaya kuwa ni wadhamini lakini wilaya hazinufaiki.
“Vipengele tata vinavyokandamiza klabu katika mikataba inayosimamiwa na TFF vitarekebishwa au kuondolewa kwa maslahi ya soka na haki za klabu katika matangazo ya biashara zitalindwa kwa nguvu zote,”alisema.
Malinzi (53) alizaliwa Agosti 8, 1960 mkoani Kagera na kupata elimu yake ya sekondari mwaka 1974 hadi 1977 Mwanza Sekondari na baadaye kujiunga na kidato cha tano na sita mwaka 1978 hadi 1981 Ilboru Sekondari.
Tangu mwaka 1999 amekuwa akijihusisha na masuala mbali mbali ya michezo ikiwemo soka na ngumi.Ni dhahiri kwamba wadau wengi wa soka watakuwa wakisubiri kwa hamu kuona Malinzi akitekeleza ahadi hizo.
Sambamba na ahadi hizo, kuna kiu ya muda mrefu ya mashabiki wa soka kutaka kuona timu yao ya taifa ikishiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na zile za Kombe la Dunia..

No comments:

Post a Comment