Saturday 26 October 2013

Taarifa Rasmi Kutoka IKULU

 
Rais Jakaya Kikwete:Tunao Wanasiasa wa Kutosha,Sasa Tunahitaji Wanasayansi.

Rais Kikwete: Kero hii imetosha, sasa ni kitabu kimoja mwanafunzi mmoja
· Asema tunao wanasiasa wa kutosha, sasa tunahitaji wanasayansi

· Aaagiza viongozi katika ngazi zote kutenga fedha za kuwajengea walimu nyumba katika bajeti zao

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake itakomesha kero ya wanafunzi na watoto wa shule nchini kuchangia vitabu vya kiada katika masomo yao.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa wajibu wa kuhimiza ujenzi wa maabara za sayansi katika shule nchini siyo tu matakwa ya Rais bali suala hili linatakiwa kuwa wajibu wa kufa na kupona kwa kila kiongozi katika ngazi zote za uongozi kwa sababu nchi haiwezi kuendelea bila wanasayansi.

Vile vile, Rais Kikwete amewaagiza viongozi wote katika ngazi zote na hasa kwenye ngazi ya wilaya na halmashauri kutenga katika bajeti zao fedha za kujenga nyumba za walimu kwa nia ya kuboresha mazingira ya kazi ya walimu nchini.

Rais Kikwete amesema na kutoa maagizo hayo jana, Jumatano, Oktoba 23, 2013, alipozungumza na uongozi wa Mkoa wa Njombe wakati anakamilisha na kujumuisha ziara yake ya siku saba katika Mkoa huo kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Rais ambaye alizungumza masuala mengi kuhusiana na aliyoyaona wakati wa ziara hiyo alijielekeza kwa muda mrefu katika masuala ya elimu na nafasi ya viongozi katika kusuma mbele sekta ya elimu kama mkombozi mkuu wa Watanzania.

Kuhusu kupatikana kwa vitabu vya kiada kwa watoto na wanafunzi nchini, Rais Kikwete amewaambia viongozi hao wa Njombe:

“Nimeilekeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi kuwasilisha kwangu bajeti inayotakiwa kutuwezesha sisi, kama Taifa, kuhakikisha kuwa kila mtoto wetu na mwanafunzi wa nchi yetu hii anakuwa na kila kitabu cha kiada kwa kila somo.”

“Hili ni jambo ambalo tumelizungumza kwa muda mrefu. Hakuwezi kamwe kuendelea kuahirisha majawabu ya suala hili. Nataka kujua itatugharimu kiasi gani kwa kila mtoto na mwanafunzi nchini kuwa na kitabu chake cha kiada kwa kila somo. Tumepata msaada wa marafiki wetu. Tunawashukuru. Lakini sasa wakati umefika kwa sisi wenyewe kuelekeza nguvu zetu zote kumaliza tatizo hilo,” amesema Rais Kikwete na kusisitiza:

“Ilikuwa wanafunzi 10 kwa kitabu kimoja, tumeshuka hadi wanafunzi watatu kwa kitabu kimoja. Hili halitoshi na hali hii haikubaliwi ni lazima iwe ni mwanafunzi mmoja na kitabu kimoja, kitabu chake.”

Kuhusu ujenzi wa maabara ya sayansi katika kila sekondari nchini na umuhimu wa kufundisha masomo ya sayansi nchini, Rais Kikwete amesema “ni lazima tujenge hizi maabara haraka, ni lazima tuongeze kasi yetu ya kufundisha masomo ya sayansi na ni lazima tukabiliane na uhaba wa walimu wa kufundisha sayansi nchini.”

“Maendeleo ya nchi huletwa na wanasayansi. Na kama mfumo wa elimu wa nchi yoyote hautoi nafasi ya kutosha kulea na kujenga wanasayansi basi nchi hiyo inapiga hatua ya kurudi nyuma. Kwenye hili, tayari tumeachwa na treni na wala suala hili siyo matakwa ya Rais bali ni suala la kufa na kupona kwa viongozi wote wa ngazi zote,” amesema Rais Kikwete.

Ameongeza: “Siyo kila mtu katika nchi yetu atakuwa mwanasiasa. Hawa tayari tunao wa kutosha na wengine kazi yao sasa ni kusababisha ghasia nchini. Tunahitaji wanasayansi zaidi – tunahitaji madaktari, tunahitaji wahandisi. Ni lazima tuwekeze ipasavyo katika eneo hili kwa sababu tukikosea sasa tutakuwa tumekosa hatua moja kubwa na muhimu katika jitihada za kujiletea maendeleo.”

Amesema kuwa anatambua matatizo yaliyoko katika ufundishaji wa masomo ya sayansi nchini na kuwa kwa sababu hiyo ameitisha mkutano wa wadau wote wanaohusika na elimu na eneo la sayansi nchini ambao utafanyika Novemba 3, mwaka huu, kwa nia ya kutafuta majawabu ya matatizo hayo.

Tanzania inahitaji walimu 44,007 wa sayansi katika shule zake za sekondari. Waliopo kwa sasa ni walimu 17,059 na hivyo kuwepo na upungufu wa walimu 26,948 wakati vyuo vyote nchini vina uwezo wa kuhitimisha walimu 2,100 kwa masomo ya sayansi kila mwaka.

Kuhusu ujenzi wa nyumba za walimu, Rais Kikwete amesema kuwa kila kiongozi popote alipo ni lazima awe na mpango kabambe wa kuhimiza ujenzi wa nyumba za walimu na kuweka katika bajeti yake ya kila mwaka fedha za ujenzi huo.

“Kwenye ngazi ya taifa tumetoa Sh. Milioni 500 kwa kila Halmashauri nchini mwaka huu kama namna ya kuanza kukabiliana na tatizo hilo. Mwaka huu wa fedha, tunaanza kwa majaribio na Halmashauri 40 na ile ya Makete katika Mkoa huu wa Njombe ni mojawapo. Tutaendelea kutoka fedha kila mwaka huu kwa nia ya kumaliza tatizo hili.”

Ameongeza: “Sasa kwenye kila ngazi ya wilaya, kaeni chini mtafakari jinsi gani ya kuzitumia fedha hizo vizuri ili ziweze kujenga nyumba nyingi. Natambua kuwa kwenye sehemu nyingine shughuli hii itakuwa ngumu unapokuwa na madiwani ambao pia ni wakandarasi. Lakini hii tutakabiliana nalo.”

Ameelekeza kuwa mbali na kuzitumia fedha hizo vizuri, pia ametaka kila Halmashauri nchini kutenga fedha katika bajeti zao za ujenzi wa nyumba za walimu.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Oktoba, 2013

No comments:

Post a Comment