Saturday 26 October 2013

Waziri Kagasheki matatani • Raia wa kigeni aliowaita majangili, walibambikwa kesi

JESHI la Polisi mkoani Arusha, limeingia kwenye kashfa nzito baada ya kubainika kumdanganya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kwa kuwahusisha raia wawili wa kigeni na biashara ya ujangili wakati si kweli.
Hatua hiyo inakuja baada ya Waziri Kagasheki kudai kuwa watumishi wa serikali wanakwamisha juhudi za kukabiliana na majangili wa tembo, akitolea mfano wa Mkuu wa Upelelezi wa Polisi mkoani hapa (RCO), Duwan Nyanda, kwamba aliwatorosha raia wawili wa Saudia ambao walikamatwa wakiwa na meno ya tembo pamoja na silaha nzito.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali na nyaraka kadhaa, Tanzania Daima limebaini kuwa raia hao waliingia nchini Septemba 12, mwaka huu, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kisha kufikia kwenye hoteli ya kitalii ya Mount Meru.
Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa wageni hao waliondoka nchini Oktoba 4, mwaka huu, kupitia uwanja huo huo.
Kwa mujibu wa waraka wa upekuzi wa polisi (search order) uliosainiwa na Inspekta James, maofisa wa jeshi hilo walifika kwenye hoteli hiyo Oktoba 3, mwaka huu, na kupekua vyumba vya wageni hao, lakini hawakukuta kitu chochote kinachohusiana na nyara za taifa za maliasili kama ilivyodaiwa na Waziri Kagasheki.
Nyaraka hiyo inaonyesha kuwa walioshuhudia upekuzi huo mbali na waliokuwa watuhumiwa, Ali na Nader, ni pamoja na Gidion David na Joseph Enock ambao waliisaini.
Tanzania Daima lilifika hotelini hapo na kuzungumza na meneja mapokezi, Enock Maselle ambaye pia alithibitisha kuwa Oktoba 3, mwaka huu, walifika polisi kwa ajili ya kukagua vyumba vya wateja wao, Ali na Nader.
Alisema kuwa waliwaruhusu, lakini akadai ni vigumu kujua nini kiliendelea.
Raia hao wanadaiwa kujihusisha na kutafuta watu nchini mwao ambao huwaleta Tanzania kutalii, na kwamba waliingia nchini na kundi la wageni tisa ambao walifanya safari kwa nyakati mbili tofauti, wakitembelea hifadhi za taifa za Manyara na Tarangire na Ngorongoro iliyopo chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Mmiliki wa kampuni ya uwakala wa utalii ya Kalabash, Ally Kalabash aliliambia gazeti hili kwa simu kuwa Ali na Nader walimletea wageni tisa ambao alifanya nao safari ya siku tatu katika mbuga za Manyara, Ngorongoro na Tarangire.
“Hawa ni mawakala wapya, na hii ni mara yangu ya kwanza kufanya nao kazi, ila wageni walioniletea niliwahudumia mpaka siku wanaondoka, kwani wengine walilala Mount Meru Hotel na wengine Themi Suite,” alisema.
Naye Salim Islam Salim ambaye ndiye alikuwa karibu na raia hao wa Saudia, alisema kuwa  walipokuwa hapa nchini walikutana na Richard Kalembe ambaye aliwaambia anamiliki kampuni ya uwindaji wa kitalii ya RS Kalembe Hunting Routes.
Alisema kuwa Septemba 14, mwaka huu, Ali na Nader walimlipa Kalembe malipo ya awali kwa ajili ya kwenda kuwinda kitalii, kiasi cha dola za Marekani 3,000.
Salim alifafanua kuwa Kalembe aliwapatia wageni hao risiti yenye namba 012 ikionyesha kuwa bado wanadaiwa dola 7,000 endapo watatumia siku tano na ikiwa watatumia siku tisa wakiwinda, basi wangelazimika kuongeza dola 9,000.
Kwa mujibu wa Salim, baada ya Kalembe kupokea malipo hayo, hakufanya mawasiliano tena na wageni hao, hatua iliyowalazimu kutoa taarifa polisi Oktoba 2, mwaka huu.
Alisema kuwa siku iliyofuata, raia hao walipigiwa simu na polisi wa upelelezi aliyemtaja kwa jina moja la James, akiwaambia kuwa mtuhumiwa wao ameshapatikana, hivyo wafike polisi ili wakakabidhiwe fedha zao.
“Katika hali ya kushangaza, walipofika polisi waligeuziwa kibao na kuwekwa chini ya ulinzi, wakitakiwa kwenda kupekuliwa kwenye vyumba vyao katika hoteli waliyofikia ya Mount Meru, ambako hata hivyo hawakukutwa na kitu.
“Baadaye walirudishwa polisi na kuelezwa sababu za kupekuliwa, kwamba walitiliwa shaka kuwa wanajihusisha na ugaidi,” alisema Salim.
Alifafanua kuwa polisi waliwaambia kuwa kutokana na tukio la kigaidi lililotokea hivi karibuni nchini Kenya, wamekuwa makini kwa kila mtu wanayemuhisi au kumtilia shaka, na hivyo humfanyia upekuzi.
Kwa mujibu wa Salim, baada ya maelezo hayo walielezwa kuwa wanaweza kuwadhamini. Yeye na mtu mwingine aliyemfahamu kwa jina moja la Ibra, walimdhamini Ali huku Nader akidhaminiwa na msichana mwingine ambaye hakumfahamu vizuri.
“Oktoba 4, tulifika pale polisi asubuhi, baada ya panda shuka, watuhumiwa hao waliwaeleza polisi kuwa wanapaswa kuondoka siku hiyo, hivyo wakaomba wapewe ruhusa wakabadili tiketi zao au wapelekwe mahakamani ili wajue wanashikiliwa kwa makosa gani.
“Tukiwa pale, akaja polisi mmoja mwanamke akasema ‘kama hawa mmewapekua mkaona hawana kitu, waachieni waende zao’. Ilikuwa kama saa tano asubuhi,” alisema.
Salim alisema kuwa wageni hao walipewa simu na hati zao za kusafiria na hivyo wakaondoka kituoni hapo, na baadaye jioni walipanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia na kurudi kwao.
Alisema kuwa alishangazwa na taarifa zilizoandikwa na vyombo mbalimbali vya habari zikiwahusisha Ali na Nader na uwindaji haramu huku wakidaiwa kukutwa na pembe za ndovu, jambo alilodai ni uongo na upotoshaji mkubwa.
Salim alisema madai ya kwamba dola 3,000 zilitolewa polisi kama rushwa si ya kweli, kwani kiasi hicho ni fedha anazodaiwa Kalembe alizochukua kwa raia hao, huku akidai taarifa iko polisi.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas kuzungumzia sakata hilo, alisema hayuko tayari kwa sababu linashughulikiwa na mkuu wa jeshi hilo, IGP Said Mwema ambaye ameunda tume ya uchunguzi.
Naye Waziri Kagasheki alipotafutwa, simu yake iliita bila kupokelewa.
Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment