Monday 28 October 2013

Manoti yakaribia mfukoni mwa Mfaransa wa Simba


KOCHA Mfaransa, Patrick Liewig, atakuwa jukwaani leo Jumatatu kuishuhudia Simba na Azam, lakini atakuwa na raha kwani uongozi wa Simba umemhakikishia kwamba keshokutwa Jumatano atakuwa tajiri kwa vile watamjaza manoti yake.
Kwa mujibu wa Liewig ambaye yupo Dar es Salaam kwa siku kadhaa sasa, anaidai Simba Sh26 milioni na amesema Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, amemthibitishia kwamba siku hiyo mambo yake yatakuwa freshi.
Liewig ambaye amegoma kuondoka Dar es Salaam mpaka atakapopata mshiko wake, alisema: “Nashukuru kuwa tumekubaliana na Simba kupitia kwa Ismail Rage na Zacharia Hans Pope kuwa watanilipa pesa zangu kama tulivyoandikishana awali.
“Natarajia mambo yaenda kama yalivyopangwa, ni vizuri kufikia mwisho.”
Liewig aliwasili Dar es Salaam Oktoba 18 na kushuhudia mchezo wa Simba na Yanga uliofanyika siku mbili baadaye uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3, Simba ikirudisha yote kipindi cha pili.
Kocha amesema akishapewa chake, atakwea pipa kurudi kwao.
Hata hivyo kuna habari kuwa anaitamani sana kazi ya kuinoa Coastal Union na amekuwa akitafuta upenyo wa kuwashawishi vigogo wa timu hiyo wampe kazi.

No comments:

Post a Comment