Monday 28 October 2013

Yaya Toure aitwa Fifa

KIUNGO wa Manchester City, Yaya Toure, amealikwa kukutana na bosi wa kitengo cha kuzuia ubaguzi wa rangi cha Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) baada ya kudokeza kwamba huenda wachezaji weusi wakagomea kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 kutokana na ubaguzi wa rangi kukithiri nchini Russia.
Toure analalamika kwamba alibaguliwa na mashabiki katika pambano la Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya CSKA ya Russia Jumanne iliyopita na huenda akawashawishi wachezaji weusi wasiende Russia kucheza Kombe la Dunia katika fainali zitakazofanyika huko.
Jeffrey Webb, ambaye anaongoza kitengo hicho cha kuzuia ubaguzi wa rangi, jana Jumapili alisafiri mpaka London, England akitazamia kuonana na Toure mara baada ya kumalizika kwa pambano kati ya City dhidi ya Chelsea.
“Naenda kwenye mechi kwa matumaini ya kupata nafasi ya kuonana na Yaya. Nimeomba kuonana naye. Nataka kujua Yaya alivyojisikia na kupata stori nzima,” alisema Webb ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Fifa.

No comments:

Post a Comment