Saturday 26 October 2013

‘Makundi jumuiya za CCM yanatutesa sana’

Dodoma. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba, amesema makundi yaliyotokana na uchaguzi katika jumuiya za chama hicho, yanawapa shida.
Nchemba aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu kwa viongozi na watendaji wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), mjini Dodoma.
Hata hivyo, Nchemba ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema UWT imetulia tofauti na jumuiya nyingine za chama hicho kikongwe cha siasa nchini.
Jumuiya nyingine za chama hicho ni Wazazi na Umoja wa Vijana (UVCCM).
“Jumuiya nyingine tunapata shida, wanaadhibiana lakini kwenu UWT, kumetulia,”alisema Nchemba.
Aliwataka UWT kuvunja makundi na kushirikiana katikia kuiendesha.
“Tangu zamani wanawake wanatabia ya kusameheana, mshirikiane na wale waliowachagua na wasiowachagua. Msiruhusu makundi,” alisema.
Alitoa mfano wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ambaye amekuwa akitoa nafasi za uongozi kwa watu wote wakiwemo waliomtukana wakati uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, alisema makundi yanayomuunga mkono mgombea katika chaguzi si dhambi, lakini yanatakiwa kuvunjwa baada ya kumalizika kwa chaguzi.
Pia aliwataka kuhakikisha kuwa wanawake wanaandikishwa katika daftari la kudumu la kupiga kura na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Naibu katibu mkuu huyo, alisema daftari hilo ni la muhimu katika maisha ya Watanzania na kwamba ni vema watu wakijitokeza kila linapofanyiwa marekebisho.
Aliwataka wajumbe kujadili kwa kina mambo yote muhimu.

No comments:

Post a Comment