Saturday 26 October 2013

Nguo za ndani za mitumba: Mkombozi wa maskini, msambaza magonjwa!

Nguo hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa Watanzania maskini, hasa wanawake kwani wakati mwingine huuzwa kuanzia Sh300 hadi Sh500.
Ni saa tano asubuhi jua linawaka, soko la Karume wilayani Ilala jijini Dar es Salaam  tayari limejaa watu wa kila rika. Kwa jumla, ni mchanganyiko au mseto wa wafanyabiashara , wachuuzi na hata wanunuzi.
Wengi waliomo ndani ya soko hilo kwa maana ya wanawake na wanaume ama wananunua au kuuza nguo , viatu chakavu ambavyo tayari vimevaliwa na watu wa nchi tajiri za magharibi. Nguo hizo ndizo zimepewa jina maarufu la mitumba.
Miongoni mwa ‘mitumba’ hiyo, ni nguo za ndani, sidiria na hata chupi za kike na kiume, ambazo zimesheheni katika meza nyingi za wafanyabiashara huku nyingine zikiwa zimetundikwa.
Ununuzi huo wa nguo za mitumba ni jambo ambalo hadi asilimia 90 ya Watanzania hasa wa kipato cha chini au kawaida wamelifanya kaitka maisha yao.
Baadhi yao wamezaliwa na kukuta utamaduni huo, nao wakauendeleza na kisha kuurithisha kwa watoto wao. Zipo sababu nyingi za wengi katika jamii kuendelea kununua na hata kuvaa mitumba, zikiwamo za kiuchumi, mazoea.
Hata hivyo,  wataalamu wa afya wanaonya na kusema kuwa nguo hizi za mitumba, hususan za ndani zina madhara mengi kwa wanawake na wanaume wanaopenda kuzitumia.
Hivi karibuni, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limepiga marufuku na kutoa kipindi cha mwisho kwa wafanyabiashara hao wanaouza nguo za ndani za mitumba, kuacha kuuza bidhaa hizo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kipindi  cha mpito kuisha, ambapo kwa sasa TBS wamechukua uamuzi wa kuzichoma moto nguo hizo. Msemaji wa TBS,  Rhoida Andusamile anasema hatua hiyo ni utekelezaji wa matakwa ya agizo la sheria ya mwaka 2009 inayozuia matumizi ya nguo za ndani zilizokwishatumika.
Profesa Malise Kaisi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Shirikishi Muhimbili (Muhas) anasema, yapo madhara makubwa ya kuvaa nguo za ndani za mitumba kutokana na unyeti wa maeneo yanapovaliwa nguo hizo.
 Anasema, walioketi juu ya hatari zaidi ni wanawake ambao maumbile yao yapo wazi zaidi na ni rahisi kwa vijidudu  kuingia kwa urahisi pindi wanapokaribia vitu hatarishi. Kwa mfano, anasema, nguo za ndani zilizovaliwa huenda zina vijidudu vya fangasi au chawa wa sehemu za siri, mwanamke anapovaa hupata maambukizi hayo.
“Endapo watavaa nguo hizo bila kuzifua kwa usahihi na kuzichemsha, kisha kuzipiga pasi, ni rahisi kupata maambukizi. Lakini pia, si vyema kimaadili kuvaa nguo zilizokwishavaliwa na watu wengine” anasema Prof  Kaisi.

No comments:

Post a Comment