Friday 25 October 2013

Madiwani wamgomea RC

BAADHI ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, wamegomea agizo la mkuu wa mkoa huo kwenye kikao cha baraza.
Madiwani hao wamekataa kusoma taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo mbele ya kikao cha baraza, wakidai kuwa jambo hilo linafanywa katika vikao vya kata na hawana sababu ya kufanya hivyo.
Walieleza kuwa pamoja na kwamba agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wao, hawako tayari kulifuata kwani hawajawahi kukaa na kujadili kuhusu watendaji wa kata kuingia kwenye mabaraza na kusoma taarifa kwa niaba yao.
“Haya mambo yanafanyika kule kwenye kata, hivyo sisi hatuwezi kusomewa taarifa za kata zetu na watendaji, kama wanataka hao watendaji wasome wao kama wao lakini sisi wasitushirikishe,” alisema John Farayo, Diwani wa Endashwod.
Hata hivyo, madiwani hao walisema kuwa mpango ulioanzishwa na mkuu wa mkoa sio mbaya ila viongozi wa halmashauri hiyo hawakutoa nafasi kwao kujadili muhtasari ulioletwa na mkuu huyo badala yake wameamua kuanzisha ghafla.
“Hatuna kanuni ya mwaka 2013 kama ilivyo taarifa na waraka wa mkuu wa mkoa na baraza la madiwani.
“Ni mamlaka hivyo hakuna zaidi yake, hivyo wajumbe wameona hawana mtu wa kumsomea taarifa hii,” aliongeza Masala Bajuta, Diwani wa Gisambalang’.
Agizo la kusoma taarifa za utekelezaji wa maendeleo lilitolewa na mkuu wa mkoa huu, Elaston Mbwilo, kwenye baraza maalumu la madiwani kusomewa taarifa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) lililofanyika Oktoba 7, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment