Saturday 26 October 2013

NANI KIPA WA KIHISTORIA SIMBA SC Mohamed Mwameja || Juma Kaseja


JUMA Kaseja alijiunga na Simba SC mwaka 2003, akitokea Moro United na aliidakia klabu hiyo hadi msimu wa 2009, aliposaini Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Baada ya makataba wake kwisha, hakuongezewa mwingine na mara moja Simba ikamsajili tena.
Kaseja kwa mara ya kwanza Simba alisajiliwa msimu ambao Mohamed Mwameja alikuwa amestaafu, akapatikana shujaa mpya wa kwenye milingoti Msimbazi, mtoto wa Kigoma, aliyekulia Morogoro, Juma K. Juma aka Juma Kaseja.

Kaseja pia, akiwa Simba katika msimu wake wa kwanza tu aliifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Kagame nchini Uganda, ambako walifungwa 1-0 kwa tabu na wenyeji SC Villa.
Msimu huo huo wa 2003, Kaseja aliiongoza Simba kuitoa Zamalek ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, miaka 10 tangu Mwameja aiongoze Simba kucheza fainali ya Kombe la CAF na kufungwa na Stella Abidjan.
Kuanzia mwaka 2004, baada ya zama za Manyika Peter, Kaseja akawa Tanzania One na hadi leo - nani mwingine zaidi yake?
Kaseja amepitia vipindi vigumu pia, kuna wakati mwaka 2007 alisimamishwa Simba kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, mambo ambayo yanakatisha tamaa na wakati mwingine yanaweza kukuondoa kwenye soka, lakini alisimama imara na alipomaliza kutumikia adhabu yake, ameendelea kuwa Simba One.
Timu ya taifa, alipokuja Mbrazil Marcio Maximo alimtema kwa sababu hizo hizo za nidhamu na hakumrejesha hadi alipoondoka na kuajiriwa kocha mpya Mdenmark, Jan Bolrge Poulsen akamrejesha kikosini.
Alirejea kwa kishindo mwaka 2010, akiiwezesha timu ya Bara kutwaa Kombe la Challenge ambalo Mwameja alilitwaa mara moja tu, 1994 nchini Kenya.
Mwameja alitwaa mataji 16 akiwa na Simba, ambayo ni ubingwa wa Ligi Kuu (matatu) 1994, 1995 na 2001, Kombe la Nyerere (mawili) 1995 na 2000, Ligi ya Muungano (matano) 1993, 1994, 1995, 2001 na 2002, Kombe la Tusker (mawili) 2001 na 2002, Kombe la Kagame (manne) 1992, 1995, 1996 na 2002 na kucheza fainali ya CAF 1993.
Kaseja hadi sasa amekwishatwaa mataji sita akiwa na Simba, ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2003, 2004, 2007 na 2010, jumlisha wa 2009 aliotwaa na Yanga, Kombe la Tusker 2003 na 2005 mawili pamoja la Kenya. Jumla Kaseja ana Medali nane za dhahabu kabatini kwake.

Tuhuma za kuihujumu Simba kwenye mechi za Yanga wote wawili zimewakumba - na Kaseja na Mwameja pamoja na kwamba klabu hiyo wamepitia makipa wengine hodari kama Omar Mahadhi, Athumani Mambosasa na Father Pazi kati yao unaweza kumpata kipa bora wa klabu daima.

No comments:

Post a Comment