Tuesday 29 October 2013

Kumekucha Azam TV

UONGOZI wa Azam TV unatarajiwa kufanya uzinduzi rasmi mwezi ujao jijini Dar es Salaam huku ukijinasibu kutoa huduma ya kiwango cha juu kwa bei nafuu ili kuwanufaisha wananchi.
Hayo yalibainishwa na Mtendaji Mkuu wa Azam TV, Rhys Torrington, wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofanya ziara katika ofisi za Azam Media jijini Dar es Salaam.
Torrington alisema wamejipanga kutoa huduma bora yenye kiwango cha kimataifa ambako wanatarajia kufanya uzinduzi rasmi Novemba mwaka huu.
Alisema, kati kati ya Novemba, wataanza kuuza ving’amuzi vya Azam TV ambako itawawezesha watazamaji kujionea zaidi ya Chaneli 30.
Alibainisha kuwa, ving’amuzi vya Azam TV vitapatikana kwa sh 95,000 na dishi lake huku huduma ya kufungiwa majumbani ikiwa ni bure.
“Mteja akishafungiwa huduma za Azam TV, malipo ya mwezi yatakuwa ni sh 12,500 tu na mteja atapata chaneli zaidi ya 50 katika king’amuzi cha Azam TV, ingawaje kwa kuanzia tutaanza na chaneli 30,” alisema Torrington.
Aliongeza kuwa, Azam TV itakuwa na Azam 1 itakayokuwa na habari za Afrika na zaidi za Kiswahili huku Azam 2 itakayokuwa ya kimataifa na baadhi vipindi vya Kiswahili na sinema za Kitanzania kwa saa 24.
Azam TV inayomiliki haki za kurusha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom hivi sasa inarusha mechi hizo kupitia TBC1, huku ikitarajiwa kuanza kuzionesha yenyewe moja kwa moja mzunguko wa pili kwa ubora zaidi.

No comments:

Post a Comment