Saturday 26 October 2013

UCHAGUZI MKUU TFF: Lowassa, Tenga watuma salamu

ALIYEWAHI kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa, amewataka wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuchagua viongozi watakaoendeleza juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika mpira wa miguu hapa nchini.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema akiwa kama mmoja wa wadau wa soka, amekuwa akifuatilia harakati za kuelekea uchaguzi mkuu wa TFF, kesho.
“Hii ni siku muhimu sana kwa soka la Tanzania. Ni siku ambayo wajumbe watatuchagulia viongozi wa kuliongoza soka letu na kuendeleza juhudi za Rais wetu Jakaya Kikwete katika kuusaidia mpira wa miguu hapa nchini,” alisema Lowassa katika taarifa yake hiyo na kuongeza: “Ningependa kuchukua nafasi hii kuwaomba wajumbe watuchagulie watu watakaoendeleza juhudi hizo, ambazo kwa hakika kila Mtanzania ameshuhudia jinsi Rais alivyojitolea kuiinua soka.
Alimpongeza Rais wa TFF anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga, kwa kuweka msingi imara katika kuliongoza soka la Tanzania.
“Soka ni mchezo unaopendwa sana na Watanzania, kwa hiyo ni lazima uongozwe kwa kufuata sheria, kanuni na katiba. Katika dunia tuliyonayo hivi sasa, soka ni sehemu ambayo ikipangiwa mikakati na utekelezaji wa maamuzi, inaweza kuchangia sana katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana wetu,” alisema.
Lowassa aliongeza kuwa anatamani kila mkoa angalau ungekuwa na shule moja maalumu kwa ajili ya soka, ambako humo vijana wataandaliwa kuwa wachezaji watakaoweza kwenda nje na kuwa wanasoka wa kulipwa.
Aliwatakia mkutano wa amani, utakaotoa viongozi imara, watakaofuata sheria, kanuni na katiba kwa mustakabali wa soka la Tanzania.
Katika hatua nyingine, naye Tenga amewataka wajumbe kutofanya makosa katika upigaji kura wa kuchagua viongozi kesho.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Tenga alisema sio muda wa wagombea kuchagua viongozi kwa kuwaangalia sura zao, bali waangalie ambaye atasaidia kuinua soka la Tanzania.
Alisema licha ya yeye kumaliza muda wake wa kuongoza TFF,  hatosita kuwasaidia kwa chochote viongozi watakaoingia madarakani.
Aidha, Tenga aliwataka viongozi ambao watafanikiwa kuchaguliwa hiyo kesho, wahakikishe wanatenda haki kwa kutumia vema kanuni na sheria ambazo zinatumika ndani ya shirikisho hilo.

Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment