Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa msimamo wake kuhusu Mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea nchini kikieleza kuwa kinaiamini na kuiheshimu Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba ambaye ni mwenyekiti.
Kauli hiyo ya CCM imekuja kipindi ambacho Jaji
Joseph Warioba akivishutumu vyama vya siasa kuingilia mchakato huo, huku
akivionya kwamba mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba yametoka
kwa wananchi, siyo vyama vya siasa.
Ufafanuzi huo wa CCM unaonekana kama kutaka kuweka
mambo sawa baada ya hivi karibuni vyombo vya habari kumnukuu Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho, Abdallah Bulembo akisema siyo
sahihi kwa Jaji Warioba kuwa msemaji wa Watanzania kuhusu mambo
wanayoyataka yaingizwe ndani ya Katiba.
Katika majibu yake, Jaji Warioba alimtaka Bulembo
kuacha kupiga kelele dhidi yake kwa maelezo kuwa hakumtuma kazi ya
kukusanya maoni ya Katiba Mpya, bali alitumwa na Serikali kwa niaba ya
wananchi
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi
Ndogo ya CCM Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho,
Nape Nnauye alisema kuwa chama hicho tawala kinaiheshimu tume hiyo na
kamwe hakiwezi kuiingilia.
Nape alisema tume hiyo iliteuliwa kwa ajili ya
kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya, hivyo wanaiheshimu na
wana imani nayo. “Tunaheshimu tume, tuna imani nayo na tunaahidi
ushirikiano wa kutosha katika mchakato wa Katiba" alisema Nape.
Kauli ya Nape imekuja wakati ambao kuna msuguano
kati ya CCM na Serikali yake kwa upande mmoja na vyama vitatu vya
upinzani vyenye wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
No comments:
Post a Comment