Umoja wa Ulaya (EU), umelaani vikali kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kwa madai ya kuandika habari zenye taswira ya uchochezi.
Taarifa ya kulaani uamuzi huo, ilitolewa leo
jijini Dar es Salaam na msemaji wa Umoja huo, Tom Vens. Taarifa hiyo pia
iliungwa mkono na mabalozi wa Canada, Norway na Uswisi.
Serikali iliidhinisha kufungiwa kwa magazeti hayo
Septemba 27 mwaka huu, huku Mwananchi likifungiwa kwa siku 14 na
Mtanzania siku 90.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, mbali na kushtushwa
kufungiwa kwa magazeti hayo, pia EU imeshangazwa na uamuzi wa Serikali
kuzuia habari kuwekwa katika mtandao wa gazeti la Mwananchi, pamoja na
kuzuia Gazeti la Rai kutoa habari zake kila siku.
“Ni wajibu wa vyombo vya habari kutekeleza
majukumu yake kwa kufuata sheria na kujitahidi kufuata maadili,”
inaeleza taarifa hiyo na kuongeza;
“Uhuru wa Habari na uhuru wa kujieleza ni haki ya
msingi kwa watu na utekelezaji wake unahitaji uangalifu na uwiano sawa
katika matumizi ya sheria zinazoongoza vyombo vya habari,” inaeleza
sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa inaeleza kuwa, haki ya kisasa ya sheria ya habari na vyombo vya habari inatakiwa kuboreshwa ili kuwa na uwazi zaidi.
“Ikumbukwe, Oktoba 2010, mapendekezo ya EU kuhusu
chaguzi huru yalieleza kuwepo na sheria za vyombo vya habari
zinazoendana na wakati wa sasa, kwa kuzingatia maoni ya wadau. Pia
ilipendekeza utaratibu bora wa kutatua migogoro na malalamiko,” ilieleza
taarifa hiyo.
Inaeleza kuwa ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya
na Tanzania unazidishwa na dhamira ya pamoja ya uhuru wa kimsingi, ikiwa
ni pamoja na uhuru wa kujieleza na habari.
“Vyombo vya habari vina jukumu muhimu la
kuuhabarisha umma kama njia mojawapo ya kukuza maadili na haki za
binadamu. Jukumu la vyombo vya habari pia ni kuendelea kuimarisha
mchakato wa demokrasia,” inaeleza.
EU unatoa wito juu ya mamlaka kufanya jitihada za kulinda uhuru wa kujieleza na kukuza haki ya kupata habari.
No comments:
Post a Comment