Monday, 7 October 2013

Herve Renard aaga Chipolopolo


Zambia imempa idhini kocha Herve Renard kuyaacha majuku yake katika timu ya taifa ya nchi hiyo ili kuchukua jukumu lake jipya la kuwa kocha wa timu ya ufaransa ya FC Sochaux.
Kocha huyo alikuwa ameanza muhula wa pili wa mkataba wake kuwa kocha wa timu ya taifa ya Zambia mnamo mwezi Oktoba mwaka 2011 na kuiwezesha Chipolopolo kufuzu kwa kombe la mataifa ya Afrika miezi minne baadaye.
Lakini Zambia ilikuwa na wakati mgumu mwaka huu kiasi cha kubanduliwa nje ya mechi za kufuzu kwa kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil.
Zambia sasa imempa kazi ya muda Patrice Beaumelle kuwa kocha wa Chipolopolo.
Beaumelle, amekuwa akifanya kazi kama kocha wa muda, na atashikilia wadhifa wa kocha mkuu wakati Chipolopolo watapocheza mechi ya kirafiki na Brazil mjini Beijing tarehe 15 Oktoba.
Shirikisho la soka nchini humo katika taarifa yake lilisema kuwa kocha "Herve Renard ameachishwa majuku yake ili kumruhusu kuiongoza timu ya Ufaransa.''
Renard, mwenye umri wa miaka 45, alichukua wadhifa huo wa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Zambia mwaka 2008 na aliiongoza timu hiyo hadi kufika robo fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2010.
Baadeya alikuwa kocha wa timu ya Angola na USM Alger kwa muda kabla ya kurejea kuwa kocha wa Zambia na kutimiza ndoto yake ya kuiongoza Zambia kunyakua kombe la taifa bingwa Afrika mwaka 2012.

No comments:

Post a Comment