Monday, 7 October 2013

Mamia ya wanafunzi wajisaidia vichakani


Shule ya Msingi Majengo, iliyopo katika Kata ya Usinge, wilayani Kaliua,Tabora, haina vyoo vya wanafunzi wala walimu tangu ianzishe mwaka 2007.
 Hayo yameelezwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Regena Luhende,  kupitia katika risala yake kwa Mbunge wa Kaliua, Prof Juma Kapuya.
Mbunge alikwenda  kukagua shughuli za maendeleo katika shule hiyo.
Mwalimu Luhende alisema  shule inakabiliwa na  tatizo la kukosa vyoo tangu kuanzishwa kwake na kwamba hali hiyo inawafanya walimu na wanafunzi wao, kujisaidia vichakani.
Aliiomba Serikali na wadau wengine wa elimu mkoani Tabora, kutoa msaada wa fedha ili kugharimia ujenzi vyoo katika shule hiyo.
Pia alisema shule yake inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati, jambo linalosababisha wanafunzi kuketi sakafuni wakati wa kusoma.
 Kwa upande wake, Profesa Kapuya alitoa mchango wa Sh3milioni   kwa shule hiyo na kuuagiza uongozi  kutumia fedha hizo, kujenga vyoo.
Alitoa wito kwa wananchi wa kata hiyo, kujenga utamaduni wa kujitolea katika kazi za maendeleo kwenye maeneo yao.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, tatizo la shule hiyo kukosa vyoo, limetokana na mwamko mdogo wa wananchi kuhusu namna ya kuharakisha maendeleo.

No comments:

Post a Comment