Monday, 7 October 2013

Mwanasoka wa Zimbabwe aliyelala Uwanja wa Ndege kwa saa 26


WANASEMA ‘ukitaka mbwa wako auawe, mpe jina baya’. Sijui. Wanasema pia ‘mdomo huumba’, pengine hilo lina ukweli kwa kisa hiki.
Unajua kimetokea nini? Wazazi wake sijui walifikiria nini, kwani mara alipozaliwa tu wakampa jina la Hardlife (Maisha Magumu).
Kwa majina yake mawili anayoyatumia ni Hardlife Zvirekwi, huyo ni kiungo mchezeshaji wa Caps United ya Zimbabwe na timu ya soka ya taifa ya nchi hiyo. Anaitwa Hardlife. Haifahamiki kwa nini aliitwa hivyo, lakini kilichomkuta mchezaji huyo kinaweza kutafsiri maana ya jina lake.
Asota uwanja wa ndege
Kwa saa 26, Hardlife Zvirekwi alisota Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, Kenya baada ya kuibiwa mabegi pamoja na pasi yake ya kusafiria. Alikuwa safarini kwenda Guinea kwa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, hivyo alilazimika kubaki uwanjani hapo akiwa hana chochote.
Hardlife si kwamba alikwama tu uwanjani hapo, bali pia aliikosa mechi muhimu huku akiishi kwa shida bila ya fedha za kujikimu, alilazimika kuishia kula mkate na kuushushia kwa maji. Alilala kwenye baridi kali la Nairobi akiwa hana shuka wala blanketi.
Apata somo
Mtaalamu wa Michezo wa Malawi aliandika siku chache baadaye katika mtandao wake wa Facebook kuhusu tukio hilo kwamba huyo si Hardlife, bali, “Hard ‘knocks’ Life.” Utani wa mwanamtandao huyo ulichukuliwa kutoka “School of Hard Knocks” ukiwa na maana kuwa vikwazo katika maisha vinaweza kumfundisha mtu.
Hardlife anaeleza kuwa tukio hilo la Nairobi limemfundisha mengi na hasa maana halisi ya jina lake, Hardlife.
Anasema aliweza kurejea Zimbabwe baada ya ofisi ya ubalozi wa nchi hiyo mjini Nairobi kumpatia hati ya dharura ya kusafiria.

No comments:

Post a Comment