Monday, 7 October 2013

MAZEMBE YA AKINA SAMATTA YASHINDA UGENINI NUSU FAINALI YA KWANZA AFRIKA

Mputu katikati alifunga bao la pili, wakati Ulimwengu kulia hakucheza kabisa na Samatta aliingia dakika za mwishoni
MABAO ya Rainford Kalaba na Tresor Mputu yameipa TP Mazembe ushindi wa 2-1 ugenini jana usiku katika Nusu Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji Stade Malien mjini Bamako, Mali.
Morikaman Koita alifunga bao pekee la wenyeji katika mchezo huo, wakati Mazembe ilipata bao la kuongoza mapema dakika ya 14 kupitia kwa Mzambia, Rainford Kalaba.

Umati wa mashabiki mjini Bamako uliduwazwa dakika tisa baadaye kufuatia vigogo hao wa Afrikan kutoka DRC kupata bao la pili dakika ya 23 kupitia kwa Tresor Mputu na dakika nne baadaye Morikaman Koita akawafungia wenyeji bao la kufutia machozi.Mechi hiyo ilikutanisha kati ya makipa wawili bora Afrika Soumaila Diakite wa Malien na timu ya taifa ya Mali, The Eagles dhidi ya Robert Kidiaba wa Mazembe na timu ya taifa ya DRC.
Mshambuliaji Mtanzania, Mbwana Samatta aliingia dakika ya 83 katika mchezo huo wakati mwenzake, Thomas Ulimwengu hakucheza kabisa.
Faida kwa Mazembe ni kupata matokeo mazuri ugenini na wakijiandaa kwa mchezo wa marudiano, wanajivunia rekodi ya kutofungwa kwenye Uwanja wao mjini Lubumbashi.
Timu hizo zinafahamiana vyema, kwani mwaka 2010 zilikutana katika Super Cup ya CAF, mwaka ambao Stade Malien walitwaa Kombe la Shirikisho na Mazembe wakiwa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa, wakashinda 2-0.
Mshindi baada ya matokeo ya jumla, atakutana na ama Bizertin au Sfaxien, zote za Tunisia ambazo jana zilitoka sare ya bila kufungana katika Nusu Fainali ya kwanza.

No comments:

Post a Comment