Monday, 7 October 2013

Wachezaji Yanga waanzisha bendi



WACHEZAJI wa Yanga wameibua kitu ambacho hauwezi kukitarajia. Kumbe huwa hawafanyi mazoezi ya kupiga pasi na chenga tu, bali pia hufanya mazoezi ya bendi kwa ajili ya kushangilia mabao wanayofunga.
Kama ni mtazamaji mzuri wa mechi za soka za Ligi Kuu Bara inayoendelea, utakuwa umegundua staili mpya ya ushangiliaji wa mabao ya wachezaji hao ambayo kumbe ina jina lake kabisa.
Wachezaji ambao mara kwa mara wamekuwa wakijumuika kwenye shoo hiyo ni Didier Kavumbagu, Jerry Tegete, Hamisi Kiiza, Simon Msuva, David Luhende na Mbuyu Twite.
Mwanaspoti ilimuuliza Msuva naye alisema: “Kwa bahati nzuri mimi ndiye kiongozi wa shoo nzima na ndiye niliyebuni aina hii ya ushangiliaji wa mabao.
“Kimsingi ni kwamba kabla ya mechi huwa tunakutana na kuchagua wimbo mmoja na kuufanyia mazoezi, lakini ni kwa yule anayetaka tu, hatumlazimishi mtu. Tutakuwa tunafanya hivi kila mechi tutakayobahatika kufunga mabao,”alisema Msuva ambaye aliwahi kuwa dansa wa kikundi cha vipaji cha Tanzania House of Talent (THT).
Kiiza yeye alienda mbali baada ya kusema kundi hilo linajulikana kwa jina la ‘Danger Zone Band’ (DZB). Staili yao ambayo imekuwa kivutio kwa mashabiki ni ya baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kujipanga mstari mmoja na kucheza mojawapo ya nyimbo za wanamuziki wa Bongo Flava hasa Diamond.
Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba, wote wamekuwa wakicheza staili moja pasipo mwingine kwenda tofauti na wenzake, hivyo kufanya ionekane kama bendi rasmi ya muziki.
Hayo ndiyo mambo ya Yanga bwana!

No comments:

Post a Comment