VIONGOZI wa Yanga nusura wazuie Kituo cha Televisheni cha Azam
kuonyesha laivu mechi baina ya Yanga na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Azam TV, ambayo ilianza kurusha matangazo yake
kupitia televisheni ya Taifa (TBC1) juzi Jumamosi baina ya Simba na Ruvu
Shooting ilijiandaa pia kuonyesha mechi ya jana Jumapili kati ya Yanga
na Mtibwa kabla ya kuzuiwa kwa muda na viongozi wa klabu ya Jangwani
Hata hivyo, Azam TV ilionyesha mechi hiyo kipindi
cha pili, licha ya viongozi wa Yanga kutishia kuwa mashabiki wao
wangefanya vurugu iwapo mechi hiyo ingeonyeshwa.
Mratibu wa Azam TV, Patrick Kahemele aliliambia
Mwanaspoti jana Jumapili jioni kuwa walifuatwa na viongozi wawili wa
Yanga (anawataja) ambao waliwazuwia wasionyeshe mechi hiyo.
“Walituambia (viongozi wa Yanga) kuwa kama
hatutaondoa kamera zetu, wangewaambia mashabiki wafanye vurugu, na
hatukutaka shari, hivyo tukalazimika kuondoa kamera zetu kwa muda,”
alisema Kahemele.
“Hata hivyo baada ya kufanya mazungumzo na uongozi
wetu wa juu wa Azam Media, wakatuambia kuwa tuonyeshe mechi kwa sababu
tupo kazini na tuna mkataba rasmi,” alifafanua Kahemele.
Kahemele alisema licha ya kuanza kuonyesha mchezo
huo kipindi cha pili hakukuwa na vurugu zozote na wamegundua kuwa
viongozi wa Yanga wamekuwa wakiwasingizia bure mashabiki wao.
Yanga wamekuwa wakigomea kusaini mkataba ambao
klabu nyingine 13 zilisaini kwa ajili ya kuonyeshwa laivu kwa mechi za
Ligi Kuu Bara na kituo cha Azam TV.
Wakati kila klabu ikipewa Sh100 milioni, Yanga
ilisusia kiasi hicho kwa madai kuwa ni fedha ndogo na hasa ukizingatia
kuwa ina mashabiki wengi nchini.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Angetile Osiah alisema watakutana kujadili suala hilo, lakini
akasisitiza kuwa Azam TV wanaruhusiwa kuonyesha mechi zote za Ligi Kuu
wanazotaka.
No comments:
Post a Comment