Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amelitaka kanisa lake na waamini kujihusisha moja kwamoja na kutafuta suluhu ya matatizo yanayoikabili dunia kwa sasa, kama alivyofanya Mtakatifu Francis wa Assisi.
Papa Francis ambaye alichukua jina hilo kutokana
na kuvutiwa na maisha ya mtakatifu huyo, alitoa wito huo kwenye ibada
maalumu ya hija ya watakatifu iliyofanyika kwenye Mji wa Assisi
alikozaliwa mtakatifu Fransis.
Alisema umefika wakati kwa Kanisa kugeuka na
kurejea misingi yake ya imani inayolenga kujali utu na kusaidia wanyonge
na wenye shida, kurejea mahitaji muhimu ya kiimani kama alivyofanya
mtakatifu huyo.
"Kanisa, sisi wote tunatakiwa kubadilika na kuacha
kukumbatia mambo maovu ya kidunia. Mambo ya kidunia ni muuaji mkubwa
kwa kuwa huua nafsi, yanaua watu na kuliua kanisa,” alisema alipokuwa
akizungumza kwa hisia kali.
“Tusipokubali kubadilika sisi wenyewe kwa sasa,
tutabaki kuwa waamini wakristo wa kibiashara, kama ilivyo keki dukani,
ambayo huwa tamu iliwapo lakini hatutaweza kuwa na matunda halisi ya
ukristo,” alisema.
Papa huyo kutoka Argentina pia alitoa salamu zake
za rambirambi kutokana na ajali ya meli iliyowakumba wahamiaji kwenye
Kisiwa cha Lampedusa huko Italia na kusababisha vifo vya zaidi ya watu
111 na wengine wengi wakiwa hawajulikani walipo.
Alisema anashangazwa na namna dunia isivyojali
kuhusu mamilioni ya watu wanaokimbia utumwa, njaa na kukimbia maeneo yao
kwa ajili ya kutafuta uhuru na namna wengi wanavyokufa kama ilivyotokea
kwenye ajali hiyo ya juzi na kusababisha vilio kwa maelfu leo.
Tunahitaji kuthamini kilio cha wale wanaobubujikwa
na machozi, wanaotaabika au kufa kwa sababu ya machafuko, ugaidi,
uharamia au vita kwenye ardhi takatifu aliyoithamini Mtakatifu Francis,
huko Syria, Mashariki ya Kati na maeneo yote duniani,” alisema Papa
Francis.
Ziara hiyo ya Francis kwenye Mji wa Assisi
inajenga dhana tofauti na waliomtangulia, John Paul II na Benedict XVI
kwa kuwa amelenga kutoa ujumbe wa kitume kuhusu kuwajali masikini zaidi
ya ujumbe wa kuhamasisha ushirikiano na mwingiliano wa kidini
No comments:
Post a Comment