Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Polisi mkoani Mbeya, Anaclet Malindisa ambaye sasa hafanyi kazi hiyo, Jumatatu ijayo anatarajiwa kutoa ushahidi wa kesi ya kusafirisha kilo 34 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh1 bilioni inayowakabili raia wawili wa Afrika Kusini, Vuyo Jack na Anastazia Cloet.
Washtakiwa hao wanadaiwa kukamatwa Novemba 18,
2010 eneo la Tunduma wakisafirisha dawa hizo kwa kutumia gari namba
CA 508650, ambapo walifunguliwa kesi ya makosa ya kusafirisha dawa za
kulevya kinyume na sheria za nchi.
Kesi yao ilianza kusikilizwa tangu mwishoni mwa mwezi uliopita na inaendelea mfululizo jijini hapa.
Tayari mashahidi wanne kati ya wanane, wameshatoa
ushahidi wao, na kwa mujibu wa Msajili wa Mahakama Mbeya, Aaron Lyamuya,
shahidi Malindisa anatarajiwa kutoa ushahidi wake Jumatatu akiongozwa
na mawakili wa upande wa mashtaka..
Upande wa mashtaka unasimamiwa na mawakili wa
Serikali, Edwin Kakolaki na Basilius Namkambe, wakati washtakiwa
wanatetewa na mawakili Ladslaus Rwekaza na Mary Gatuna.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya,
Noel Choja aliahirisha kesi hiyo, Alhamisi iliyopita hadi Jumatatu
akisisitiza umuhimu wa kuzingatia muda wakati wote wa kesi hiyo, ambayo
ni kubwa kuliko kesi nyingi zilizowahi kufanyika mkoani hapa kuhusu dawa
za kulevya.
No comments:
Post a Comment