Waziri
Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, amesema baadhi ya wabunge wa
upinzani, wameugeuza ukumbi wa Bunge kama sehemu ya malumbano, matusi
badala ya kujenga hoja ambazo zitachochea maendeleo kwa wananchi.
Bw. Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam juzi katika mahojiano maalumu na Majira juu
ya maoni yake kuhusu madai ya upinzani wanaotaka Rais Jakaya Kikwete
asisaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba mwaka 2013.
Alisema
upo umuhimu wa wabunge hao kutii kanuni za Bunge ambalo ni chombo
kinachoheshimika badala ya wabunge hao kupotosha maana nzima ya Bunge
kwa ajili ya malumbano.
"
Vyama vya upinzani vinashindwa kutumia fursa walizonazo ndani ya Bunge
ili kujenga hoja ambazo zitachochea maendeleo ya wananchi badala yake ni
watu wa kupinga na kukashifu hoja zenye tija kwa jamii," alisema Bw.
Sumaye.
Akizungumzia
suala zima la tozo ya laini kila mwezi, Bw. Sumaye aliitaka Serikali
kuangalia uwezekano wa kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili kupunguza
makali ya maisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Wakati huo huo,
Bw. Sumaye amelaani vikali hatua ya baadhi ya viongozi wa vyama vya
upinzani, kutaka Rais apunguziwe madaraka ya kuteua viongozi.
"Rais
anastahili kubaki na mamlaka hayo kwa kuteua baadhi ya viongozi kama
Waziri Mkuu, Baraza la Mawaziri, Gavana wa Benki Kuu, Jaji Mkuu, Wakuu
wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wengineo," alisema Bw. Sumaye.
No comments:
Post a Comment