Thursday, 17 October 2013

USALAMA ‘FEKI’ ANASWA MTEGONI


 Watu wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya utapeli , huku mmoja akitumia kitambulisho kinachomtambulisha kuwa ni ofisa mwandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa, wametiwa mbaroni jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo ambalo liligusa hisia za watu wengine lilitokea juzi maeneo ya Kawe, wakiwa katika Hoteli ya Picol Beach saa 2.30 siku baada ya kuwekewa mtego.
Watuhumiwa hao watanashati waliokamatwa katika tukio hilo wametambuliwa kuwa ni Fadhili Hamisi Mafutari ambaye anadaiwa kutumia kitambulisho cha Idara ya Usalama wa Taifa, kikiwa na jina la Kennedy Magige na picha yake.
Pia anatumia simu yenye namba 0654-084-445 iliyosajiliwa kwa jina la Kennedy Magige, ingawa rafiki yake ambaye amekamatwa naye kwenye tukio hilo, Tabula Abdallah Mayenga, alisema anamfahamu na jina lake, Fadhili Hamisi Mafutari.
Watu hao walikamatwa baada ya kuwekewa mtego na watu wanaodai kutapeliwa na Mayenga katika tukio lililotokea Ijumaa, wiki iliyopita maeneo ya Maua Resort Beach.
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa mashuhuda alisema baada ya kutapeliwa, walianza kuweka mtego na kufanikiwa kumnasa Magige, kwa kutumia mtu mwingine aliyempigia simu na kujifanya ana shida naye.
Mtoa habari wetu huyo, alidai kwamba wakati Magige anawafanyia tukio hilo la utapeli, hakuwa anafahamu k ama wamebaki na namba yake simu na baada ya kufuatilia, walibaini imesajiliwa kwa jina la Magige.
“Alipopigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwake pengine alidhani amekutana na mjinga mwingine, hivyo walipanga wakutane Hoteli ya Picol Beach,” alisema mtoa habari wetu.
Vyanzo vyetu hivyo, vilieleza kuwa Magige alifika hotelini hapo akiwa na gari aina Land Cruiser Prado namba T445 BCY na kisha kukutana na mtu aliyekuwa amepanga naye, bila kujua alikuwa anaingia mtegoni.
Baada ya kufika, alitiwa mbaroni pamoja na mwenzake na kuanza kushushiwa kipigo kikali na wananchi wenye hasira, ambapo ilibainika anamiliki kitambulisho kinachomtambulisha kuwa ni ofisa mwandamizi Idara ya Usalama wa Taifa.
Lakini alipohojiwa, Magige alijitambulisha kuwa yeye ni mfanyabiashara wa mazao aina ya nafaka kauli ambayo ilitofautiana na rafiki yake ambaye alikamatwa naye kwenye tukio hilo, kwani alisema Mafutari (Magige) ni mfanyabiashara wa magari.
  Mayenga alisema yeye ni fundi seremala na kwamba alifika hotelini hapo kufuata hela kidogo kwa rafiki yake,lakini ghafla aliona watu wanaanza kumfuatilia na hakuwa na njia ya kukimbia kwani alihisi ataitiwa mwizi.
  Baada ya watu hao kupata kipigo kutoka kwa wananchi, walifika Polisi ambao waliweza kubaini kitambulisho hicho cha usalama wa taifa, lakini Magige alipohojiwa alikana kuwa si mali yake.
  Watuhumiwa hao waliondolewa eneo la tukio kwa kutumia gari la Polisi namba T 332 ANV aina ya Land Rover Difender.Akisimulia tukio la kutapeliwa na mtu huyo, anayedaiwa kuwa usalama, shuhuda mmoja alisema akiwa na dada yake Ijumaa iliyopita maeneo ya Maua Resort Beach, Kunduchi alifika mtu huyo, ambapo alijifanya kama anawafahamu hivyo wakawa wamekaa wote.
  Mtu huyo, alianza kuwauliza habari za siku nyingi yeye na dada yake, wakati huo wakinywa soda. Alisema mtu huyo, inasemekana aliwawekea kitu kinachodhaniwa ni dawa za kulevya kwenye kinywaji chao, kwani hali zao zilibadilika.
  Alisema dada yake huwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo, hivyo ghafla alianza kuhisi miguu kumwishia nguvu, ndipo alipowaambia aende kwenye gari yake ili apate kiyoyozi na walifanya hivyo.
  Shuhuda huyo alisema Magige alianza kuwauliza kama wana kadi za ATM, kwani yeye hana, lakini kuna mtu anataka kumtumia fedha kutoka Arusha. Walipomwambia itawezekanaje muda huo usiku, aliambiwa kuwa Arusha wanachelewa, ndipo walikataa na hapo kuanza kumtilia shaka.
  Baada ya hapo, shuhuda huyo anaeleza kwamba alianza kumpora dada yake vitu alivyokuwa navyo na kurudisha gari nyuma kwa kasi na kuanza kuondoka na ndugu yake huyo. Alisema na yeye alikuwa na gari, hivyo alianza kumfukuzia lakini alipofika maeneo ya Mtongani, aliishiwa nguvu, hivyo ilibidi aende kutoa taarifa Polisi Mtongani.
  Alisema mtuhumiwa huyo,alienda na dada yake hadi maeneo ya hoteli moja (jina tunalo), ambapo alitaka kumtelekeza, lakini alipiga kelele kuomba msaada ambapo walianza kulifukuza gari hilo kwa Bajaj, lakini alifanikiwa kuwaacha, hivyo ndipo alipokumbuka namba na kuwapigia na kukutana nao Polisi, Mtongani.
  Alisema tangu wakati huo walianza kuweka mtego wa kunasa matapeli hao, hadi jana walipotiwa mbaroni. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillus Wambura, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, simu yake ilikuwa inaita bila kupokewa.

No comments:

Post a Comment