Siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema dawa ya kudai Katiba Mpya haitafanikiwa kwa maandamano na vurugu huku akipendekeza itumike njia ya mazungumzo na kukubaliana kwa pamoja, wasomi nchini wamevitaka vyama vya upinzani kutumia busara na kukubali ushauri huo.
Oktoba 10 mwaka huu, viongozi wakuu wa vyama vya
NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF wamepanga kufanya maandamano nchi nzima
kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa
2013, uliopitishwa wakati wa mkutano wa 12 wa Bunge mwezi uliopita kwa
maelezo kuwa una kasoro.
Katika hotuba yake ya kila mwezi kwa wananchi aliyoitoa juzi,
Rais Kikwete alisema kuandamana nchi nzima au
kuchukua hatua za kutokutii sheria kama Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe anavyotaka hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hiyo.
Alishauri utumike utaratibu kama ule wa mwaka
2012, ambapo baada ya kuibuka kwa mazingira ya kutokuelewana katika
suala la katiba, pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja
baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na baada ya kuridhiana
hatua zipasavyo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti
leo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa
Gaudence Mpangala alisema ni jambo la busara kwa Rais Kikwete kuonyesha
kutaka suluhu katika mvutano uliopo sasa.
“Najua wazi kuwa ni vigumu kwa Rais kukubaliana na
wapinzani, lakini kitendo cha kuonyesha nia ya kutaka kukutana nao na
kuweka mambo sawa kinaleta ishara nzuri,” alisema na kuongeza:
“Binafsi natambua kuna mambo hayakwenda sawa
katika upitishwaji wa muswada ule, lakini hilo linaweza kumalizwa kama
pande zote zikikutana, wapinzani wajaribu kutafakari kuhusu jambo hili.”
Naye Bashiru Ali alisema: “Inategemea…, sijui kama
wanasiasa wataamini kauli iliyotolewa na Rais Kikwete, lakini
wanatakiwa kutambua kuwa Rais ameonyesha nia ya dhati na hekima ya
kutaka kuweka pembeni tofauti zilizopo sasa.”
Aliongeza: “Nakubaliana na Rais kwamba mchakato wa
kupata Katiba Mpya hauwezi kufanikiwa kama malumbano yaliyopo sasa
yataendelea. Wanasiasa waonyeshe dhamira kwa kuweka masilahi ya taifa
mbele, lakini wakikaidi na kuendelea na mipango yao wataharibu mchakato
mzima.”
Kwa upande wake Profesa Chris Peter Maina ambaye
yupo nchini Ujerumani, alisema hotuba ya Rais imetoa msimamo wake kuhusu
mchakato wa Katiba Mpya, “Kitendo cha yeye kukubali kuzungumza na
wapinzani ni kizuri na kitaleta suluhu ya kudumu.”
No comments:
Post a Comment