Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu amesema hotuba ya kila mwezi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa siku tatu zilizopita, imejaa maneno mengi ya kuambiwa hasa kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, ikiwa ni pamoja na uteuzi alioufanya wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika
ofisi za makao makuu wa Chadema, Lissu alisema kauli zilizotolewa na
Rais za kumshutumu yeye (Lissu) kuzungumza uongo bungeni, kuhusu uteuzi
wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba zilikuwa zakuambiwa, hazina
ukweli wowote.
“Pengine rais Kikwete angesoma hotuba yangu niliyoitoa bungeni asingezungumza vile kuhusu mimi.”
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alimshutumu Lissu
kwa kusema kwamba katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kuwa Rais hakuheshimu mawazo ya Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).
Rais Kikwete alisema kauli hiyo ya Lissu ni
uzushi, uongo na uzandiki wa hali ya juu huku akisisitiza kuwa Lissu
alitoa kauli hiyo ili kupotosha ukweli na pengine isaidie kujenga hoja
yake ya kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa Bunge Maalum la Katiba.
Katika maelezo yake ya jana, Lissu alisema kuwa
alipinga Rais kuteua wajumbe wa Bunge la Katiba kwa sababu hata wakati
akiteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kupelekewa
majina na taasisi mbalimbali, alifanya uteuzi wa watu ambao
hawakupendekezwa na taasisi mbalimbali, ikiwemo TEC na CCT.
Lissu ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria
na Utawala alisema kamati hiyo ilipokutana na wawakilishi wa TEC na CCT
(majina yanahifadhiwa kwa kuwa hatukuwapata kuthibitisha hilo),
wawakilishi hao walikiri wazi kuwa majina waliyoyapendekeza sio ya watu
walioteuliwa na Rais.
“Sasa hapo uongo na uzandiki wangu ni nini, labda
hao wawakilishi wa TEC na CCT walisema uongo, hata wawakilishi wa
Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania nao waliieleza kamati kuwa
majina waliyoyapendekeza, sio ambayo Rais aliteua” alisema Lissu.
Alisema kuwa Rais amemshutumu bila kuujua ukweli,
kusisitiza kuwa kama angesoma hotuba yake aliyoisoma katika mkutano wa
12 wa Bunge, asingezungumza maneno hayo dhidi yake.
“Ndio maana katika hotuba yake rais Kikwete
alikiri wazi kwa kusema, nimeambiwa, nimesikia, nimeelezwa ukweli ni
kwamba wasaidizi wake wamemdanganya,” alisema Lissu.
No comments:
Post a Comment