Tuesday, 20 August 2013

AZAMU WAMNYEMELEA MBUYU TWITE


YANGA ikiteleza kidogo tu itapigwa bao la maana na Azam. Klabu tajiri ya Azam FC imeanza kumnyemelea kwa siri kiraka Mnyarwanda, Mbuyu Twite.
Mbio za Azam kumwania Twite zilionekana mara baada ya kumalizika kwa mechi ya Ngao ya Jamii baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Mwingereza Stewart Hall aliachana na wachezaji wote wa Yanga akaenda moja kwa moja alipokuwa, Mbuyu na Mrundi Didier Kavumbagu.
Alimsalimia Kavumbagu na baadaye akaenda kwa Mbuyu na kuzungumza naye kwa muda mrefu.
Ingawa Mbuyu hakutaka kuzungumza lolote kuhusiana na hali hiyo, lakini mtu wake wa karibu alisema Azam inamtaka mchezaji huyo na Hall alikuwa anamuuliza mkataba wake unamalizika lini na alipomjibu bado mwaka mmoja akaahidi kumpigia simu baadaye wazungumze kwa kina.
Mbuyu alisema: “Alikuwa ananipongeza kwa mchezo na mambo mengine (huku akicheka).”
Mwanaspoti ambayo lilikuwa pembeni likishuhudia kila kilichokuwa kinaendelea, lilimnasa Stewart akashtuka na kusema:  “Nilienda kumpongeza tu sawa na nilipofanya kwa wachezaji wengine wa Yanga.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Bin Kleb alisema:  “Kama kuna timu inamwania mchezaji wetu yeyote si halali kwa sasa kwa sababu wachezaji wetu wote wana mikataba zaidi ya miezi sita.”
Chanzo Mwanasipoti.

No comments:

Post a Comment