CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera, kimetetea uamuzi uliofikiwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho Mkoa wa kuwafukuza uanachama madiwani nane na kudai kuwa, uamuzi huo utaendelea kuheshimiwa.
Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Bi. Constancia Buhiye, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari siku chache baada ya Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa chama hicho Taifa, Bw. Nape Nnauye, kusema uamuzi huo hauna baraka ya vikao vya ngazi ya juu katika chama hicho.
Bi. Buhiye alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni ya CCM, Halmashauri Kuu ya chama hicho ndiyo kikao cha mwisho katika maamuzi ya kuwawajibisha wanachama wake ngazi ya Mkoa.
Alisema maamuzi yaliyofikiwa na Halmashauri Kuu ya CCM mkoani humo ya kuwafukuza uanachama madiwani hao ni halali na yataendelea kuheshimiwa hadi hatua nyingine zitakapofikiwa kama rufaa ya madiwani hao au ushauri wa vikao vya juu.
"Kwa kutumia katiba hii na kanuni hii, Halmashauri Kuu ya CCM ni chombo chenye haki ya kusimamisha uanachama wanachama wake," alisema Bi. Buhiye.
Aliongeza kuwa, vikao vya juu katika maamuzi yake pia vitarejea katiba na kanuni ya chama na kuwataka wana CCM Mjini Bukoba kuwa watulivu, wavumilivu na kuheshimiana ili kuepuka suala zima la uvunjifu wa amani.
"Mimi sipingani na Nape na sitaki kuamini niliyoyasikia kutoka kwa watu wengine maana mimi binafsi sikusikia lakini katika katiba yetu, hakuna kikao kinachofuta maamuzi ya kikao kingine, kila kikao ni halali," alisisitiza Mwenyekiti huyo.
Aliongeza kuwa, "Halmashauri Kuu ni kikao halali na maamuzi ni halali ambayo yataendelea kuheshimika." alisema na kudai kuwa, baada ya kikao hicho maamuzi yaliachwa kwa Mtendaji Mkuu wa chama ili kuandaa taarifa iweze kutumwa katika ngazi husika na kuwapatia barua madiwani hao.
Alisema hadi sasa ofisi yake haina taarifa za maandishi zilizotolewa na viongozi wa ngazi za juu kuhusu suala hilo.
No comments:
Post a Comment