Sunday 18 August 2013

Mvietnam adakwa na pembe za ndovu uwanja wa ndege













Raia wa Vietnam, anashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukutwa na shehena ya pembe za ndovu ya kilo 19 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Mtu huyo amekamatwa wakati bado suala la watu kukamatwa na dawa za kulevya likiendelea kurindima. Julai 5 mwaka huu, wasichana wawili Agnes Gerald (Masogange na Melisa Edward ) walipitisha kilo 180 za dawa hizo na kwenda kukamatiwa Afrika Kusini.
Agosti 14 mwaka huu pia mtu mmoja alikamatwa akiwa na kete 86 za dawa za kulevya aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Deusdedit Kato alisema, raia huyo alikamatwa juzi jioni akiwa anatokea Msumbiji na ndege ya Air Mozambique na alikuwa katika harakati za kubadilisha ndege ili apande ndege ya Dubai.
“Jana (juzi) majira ya saa 10:45 alasiri hapa uwanja wa ndege, alikamatwa raia wa Vietnam akitokea Msumbiji na ndege ya Shirika la Ndege la Mozambique Airlines… alikuwa katika harakati za kubadilisha ndege ili apate ya kwenda Vietnam kupitia Dubai, ndipo maofisa wetu wa polisi, uwanja wa ndege na maliasili wakamshtukia,” alisema na kuongeza: “Ilikuwa ni kwa ‘physical inspection’ (uchunguzi wa macho), aliweza kugundulika.
Baada ya kufanyiwa upekuzi wa kina katika begi lake alikutwa na bangili 138 na vijiti 362 vilivyotengenezwa kwa pembe za ndovu. Vyote vina uzito wa kilo 19 na thamani ya Sh18.4 milioni.”
Hata hivyo, alisema kuwa jitihada za kumhoji mtuhumiwa bado zinaendelea kwa kuwa hajui lugha ya Kiswahili wala Kiingereza.
“Bado tunatafuta mkalimani ili tumhoji kwa kina halafu atafikishwa mahakamani. Sheria inaruhusu mtu kushtakiwa popote anapokamatiwa, siyo lazima tumrudishe Msumbiji au kwao Vietnam,” alisema Kato. Akizungumzia hali ya ulinzi uwanjani hapo, Kato alisema kuwa imeimarishwa na kwamba ukitokea uhalifu huwa ni wa kupangwa tu.
“Siku zote tunawakamata wahalifu kama hawa, ikitokea kama ule mzigo wa mabegi tisa ya dawa za kulevya, haina maana kwamba ulinzi ulilegea, watu walijua kitu kinachoendelea. Sasa ndiyo tunajiuliza, kwa nini walijua halafu wakanyamaza,” alisema Kato.

No comments:

Post a Comment