Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, amesema tuhuma alizopewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa, za kutetea wahalifu wa mazingira, ni uongo na zinazotokana na moyo wake wa kutetea wanyonge.
Kauli ya Rutabanzibwa imekuja ikiwa ni siku moja tangu Waziri Huvisa kumtaja akimtuhumu kumkingia kifua, Robert Mugishagwe anayemiliki kiwanja Na.2002 eneo la Kawe Beach, Dar es Salaam.
Akijibu madai hayo ofisini kwake Dar es Salaam jana, Rutabanzibwa alisema hakukosea kumwekea dhamana Mugishagwe na kwamba, anazo nyaraka zinazoonyesha uhalali wa kiwanja chake.
“Nimekuwa Katibu mkuu wizara kwa zaidi ya miaka 17, nimekuwa nikizushiwa tuhuma nyingi na nimechunguzwa sana, lakini zote hazina ukweli. Hata tuhuma hizi ndiyo hizohizo za kuzusha,” alisema Rutabanzibwa na kuongeza:
“Waziri aliagiza Mugishagwe akamatwe tangu Januari, nilikwenda Kituo cha Polisi Kawe, nilipowauliza kosa lake wakasema waziri ameagiza akamatwe. Nilimdhamini ili akalale nyumbani siyo mahabusu. Kumdhamini mtu ni kosa? Nilimdhamini ili kama atapotea nikamatwe.”
Huku akionyesha barua ya polisi yenye kumbukumbu Na.KW/K/BI/1/VOL/48, Rutabanzibwa alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilipitia jalada la NEMC na kuthibitisha Mugishagwe anamiliki kiwanja hicho kihalali.
“Nilitarajia kwamba baada ya kumkamata, watafungua kesi mahakamani, mbona hawajamfungulii kesi tangu Januari?” alihoji Rutabanzibwa na kuongeza:
“...Hayo ni matumizi mabaya ya madaraka. Ndiyo maana nilimdhamini, siyo kwa sababu yeye ni Mhaya, ila natetea watu wote.”
Huku akiendelea kuchambua nyaraka zake, Rutabanzibwa alionyesha barua iliyotoka Ofisi ya Makamu wa Rais yenye kumbukumbu BA/78/27/01/61 yenye taarifa ya mgogoro wa ardhi na mazingira eneo la Kawe Beach, Dar es Salaam na kwamba taarifa hiyo inathibitisha uhalali wa kiwanja hicho.
“Pale kuna watu wengi walioingilia mto na kuna raia wa kigeni ameuhamisha kabisa wakati hana hata hati ya kumiliki kiwanja hicho, lakini haguswi. Badala yake wanambana tu Mugishagwe. Siwezi kuona mtu anaonewa halafu nikae kando, utakuwa ni unafiki. Lazima nipambane hadi haki ipatikane.”
Alipoulizwa kwa nini asimfuatilie huyo mgeni, aliyedai kuwa ametembeza rushwa kwenye wizara hiyo, alijibu:
“Hapa nina kesi nyingi za rushwa nazifuatilia Takukuru, hata wiki hii nilikuwa shahidi kwenye kesi ya wizi hapa wizarani. Isitoshe hicho kiwanja alipewa kabla sijaingia wizara hii. Lakini kuna rushwa ilitembea hapa wizarani.”
No comments:
Post a Comment