Kamati za Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Serikali za Mitaa (LAAC), Bajeti, pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimependekeza kutungwa kwa sheria ya kufilisi mali za watu watakaobainika kutafuna mali za umma.
Hayo yalielezwa jana na Naibu Spika, Job Ndugai wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufunga mafunzo ya Kamati hizo yaliyoandaliwa na ofisi ya CAG, kufafanua kuwa sheria zilizopo haziwabani wanaotafuta fedha zinazotokana na kodi za wananchi, ni vyema sasa kukawa na sheria ya kufilisi mali zao.
“Ni kweli sheria zetu zimekuwa haziwabani watu wa aina hii, wazo la kufilisi wanaotafuna mali za umma ni moja kati ya maazimio 24 ya Kamati hizi zilizopata mafunzo kwa siku tano” alisema Ndugai na kuongeza;
"Watu wamekuwa wakifungwa kwa muda na baadaye kuachiwa, hiyo ni changamoto kubwa ambayo ipo kwa sasa, huo ni mjadala wa wote ambao unahitaji jibu la pamoja.”
Alisema hata mfumo wa sasa wa jinsi Kamati za fedha zinavyoisimamia serikali katika matumizi hauko sahihi, kutokana na ukaguzi wa hesabu za serikali hufanyika baada ya fedha kutumika.
“Hii ina maana kwamba kamani madhara yatatokea fedha zinakuwa zimeshaliwa na wakati huohuo huduma iliyopaswa kutolewa inaweza isitolewe ama itolewe kwa kiwango cha chini” alisema
Alisema mfumo huo ni tofauti na ule wa Marekani ambapo bunge lake lina nguvu ya kudhibiti matumizi ya fedha kabla hayajafanyika au kukagua fedha katika mwaka huohuo, kusisitiza kuwa hiyo ni tofauti na Tanzania ambapo fedha zinazokaguliwa zinakuwa za mwaka mmoja au miwili iliyopita.
“Wakati umefika sasa wa bunge kuwa na utaratibu kama wa Marekani ili kuondoa ubadhilifu na kuleta usimamizi tija katika matumizi ya fedha za umma” alisema Ndugai.
No comments:
Post a Comment