Tuesday, 20 August 2013

Huenda kiongozi wa Boko Haram 'amekufa'

Abubakar Shekau, Kiongozi wa Boko Haram
Huenda kiongozi wa kundi la Boko Haram nchini Nigera, Abubakar Shekau aliuawa na maafisa wa usalama katika ufyatulianaji wa risasi. Duru za kijeshi zinasema huenda Shekau aliuawa kati ya Julai 25 na Agosti 3.
Kundi la Boko Haram ambalo limekua likiendesha maasi Kaskazini mwa Nigeria tangu mwaka wa 2009 halijatoa taarifa yeyote. Marekani ilitangaza tuzo ya dola Milioni saba kwa yeyote yule angepeana taarifa za kumnasa Shekau.
Taarifa za kijasusi zinasema Shekau alipigwa risasi Juni 30 wakati jeshi la Nigeria liliposhambulia maficho ya Boko Haram katika msitu wa Sambisa Kaskazini Mashariki mwa nchi.
Shekau alipata majeraha mabaya na kuvukishwa hadi katika mji ulioko mpaka na Cameroon kwa matibabu. Inaaminika alikufa kati ya Julai 25 na Agosti tatu mwaka huu. Waandishi wa habari wamesema hakuna taarifa huru ambazo zimethibitisha kifo cha Shekau.
Maelfu ya raia wameuawa tangu Boko Haram kaunza maasi mwaka 2009. Abubakar Shekau alichukua uwongozi wa wapiganaji hao wa kiisilamu baada ya kifo cha mwanzilishi wa Boko Haram, Muhammad Yusuf aliyefariki dunia wakati akiwa kizuizini.
Kundi hilo limeendesha mashambulizi mabaya na ya kikatili wakati wa uwongozi wa Shekau. Boko Haram wamekuwa wakishinikiza kuunda taifa la Kiisilamu nchini Nigeria.
Hapo mwezi Mei mwaka huu Rais Goodluck Jonathan alitangaza hali ya hatari katika majimbo matatu Kaskaizni mwa Nigeria ambapo pia alituma jeshi kuendesha operesheni dhidi ya wapiganaji hao.

No comments:

Post a Comment