Sunday 18 August 2013

Mikopo ya nyumba yaja


Sekta ya ujenzi wa nyumba inazidi kupata ahueni baada ya Benki ya CRDB kuzindua mkopo maalumu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba uitwao ‘Jijenge’, utakaokuwa mfumbuzi wa tatizo la changamoto zinazowakabili Watanzania katika ujenzi wa nyumba. 
Jijenge inatarajiwa kutatua tatizo la ujenzi wa nyumba, ununuzi wa vifaa vya ujenzi au ukarabati wa nyumba ambapo watu binafsi huwachukua hata miaka 10. Tofauti na mkopo wa nyumba wa awali uliokuwa ukilipwa kwa miaka mitano, mkopo wa Jijenge utalipwa kwa kipindi cha miaka 20, kwa riba ya asilimia 18 na asilimia 1 ya mkopo ikiwa ni kwa ajili ya bima.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei alisema wakati umefika kwa Watanzania kuishi maisha marefu ndani ya nyumba zao wenyewe kwa amani.
“Kumiliki nyumba kunatosheleza hitaji muhimu sana la mwanadamu na kumpa heshima na utulivu wa fikra na maisha. Nyumba bora ni hitaji la muhimu kabisa kwa binadamu kama ilivyo chakula na mavazi. Jijenge pia itawahudumia wale watakaohitaji mkopo huo kwa ajili kukarabati nyumba,” alisema Dk Kimei. Kimei alisistiza kuwa mkopo huo utawafaa wafanyakazi wasio na kima cha chini ya 200,000, wafanyabiashara, wakulima na wavuvi, hata hivyo alibainisha kuwa ni nyumba 15,000 tu zinajengwa kwa mwaka tofauti na hitaji la nchi.
Alisema kumekuwa na changamoto nyingi zinazokwamisha ujenzi nchini ikiwemo kupanda kwa gharama za kumiliki ardhi, gharama za vifaa vya ujenzi na kukosekana kwa mfumo thabiti wa kifedha wa kusaidia sekta hiyo.
Chanzo Mwananchi

No comments:

Post a Comment