Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku amesema asingekubali kushiriki katika Tume hiyo laiti kama angejua CCM ingeingilia mchakato huo.
Butiku ambaye alitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti, wikiendi iliyopita kwenye Mabaraza ya Katiba ya Halmashauri ya Mji wa Soni, Lushoto na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, alieleza kutokufurahishwa kwake na kitendo cha CCM kushinikiza maoni yake mbele ya mabaraza hayo.
Alilalamika kuwa kitabu cha mwongozo wa utoaji maoni kilichotolewa na CCM kinatumiwa vibaya kushinikiza maoni kwenye Rasimu ya Katiba Mpya.
“CCM imeandaa kitabu kizuri kweli kusaidia wanachama wake, tuliwaambia (Tume) hatukitaki; ni mwongozo kusaidia wanachama wake namna ya kutoa maoni, lakini kimekuwa kinatumika vibaya. Kinatumika kushinikiza maoni,” alisema Butiku.
Butiku ambaye ni mwanachama wa Tanu tangu mwaka 1958 na CCM kuanzia 1977 alisema: “Ningejua itatokea chama kitafanya hivyo, nisingekula kiapo nilichokula kufanya kazi hii katika Tume ya Marekebisho ya Katiba. Kundi moja lisigeuke Tanzania. Mimi ni mzee nasema kitu kikubwa nataka Mwenyekiti (wa CCM) asikie, Halmashauri Kuu yangu (ya CCM) isikie. Mchakato huu usiingiliwe, madiwani saidieni wananchi wenu kujielewa. Muungano hautaponywa kwa helikopta zinazoruka au vitabu vinavyosambazwa.”
Muungano
Kuhusu Muungano, Butiku aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini alisema: “Mimi ni mzee sasa, sitaki kwenda kaburini bila kuwaambia ukweli. Endeleeni kuujadili, msifanye jambo la kutaka asali bila kujua madhara yake,” alisema.
Kauli hiyo ya Butiku ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere ilitokana na wajumbe kuonyesha mvutano kuhusu muundo wa Serikali katika Muungano na wengi walionekana kuelemea upande wa Serikali mbili uliopo sasa, baadhi kuunga mkono Rasimu ya Katiba inayopendekeza Serikali tatu, huku wachache wakitaka Serikali moja.
Butiku aliwataka wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kutoa maoni yanayolenga kulinda na siyo kuvunja Muungano na kwamba Tume ya Marekebisho ya Katiba imepewa kazi ya kuulinda akisisitiza kwamba haikuwa, wala haina ajenda ya kuvunja.
“Wapo pia viongozi wakubwa ndani ya Baraza la Wawakilishi, wengine wamestaafu, hawautaki Muungano. Tume inawafahamu wanaotaka Tume ya Katiba iwe na ajenda ya kuvunja Muungano. Muungano huu, ulimfukuza Aboud Jumbe madarakani, kiongozi mkubwa tu, mi nawaambia mambo mengine siri. Jumbe alitoka kwenye mkutano wa CCM, kaja pale nje akakuta gari lake lingine siyo la Makamu. Leo, (anamtaja kiongozi huyo) anasema tulifanya makosa kuungana, anajiunga na Jumbe, anaanza kufanana na Uamsho,” alisema Butiku.
Butiku aliifananisha Katiba Mpya nzuri kuwa sawa na asali akieleza kuwa inahitaji umakini wakati wa kuiandaa, akifafanua kuwa unapoandaa asali lazima uwe makini vinginevyo unaweza kuambulia kushambuliwa na nyuki.
“Wajumbe msipokuwa wa kweli, badala yake watu wakaumwa na nyuki, mtatulaumu. Ukweli wanaufahamu wote ili waweze kuamua? Tumekubaliana kwenye Tume tuambiane ukweli ili tupate asali.”
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment