Monday, 19 August 2013

Trafiki anayedaiwa kuwa ni feki alivyokamatwa Dar





Siri imefichuka ya jinsi gani mtu ambaye aliyejifanya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, James  Juma Hussein (45), alivyokamatwa wakati akiwa ‘kazini’ eneo la Kinyerezi Mnara, Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi na kuthibitishwa na mmoja kati ya askari walioshiriki katika kumkamata zinabainisha kuwa mtuhumiwa huyo ambaye anatarajiwa kupandishwa kizimbani leo (Jumatatu), alitiwa mbaroni baada ya kulisimamisha gari binafsi la mmoja kati ya makamishna wa polisi.
Inadaiwa kuwa siku ya tukio askari huyo alisimamisha gari la bosi huyo wa polisi ambaye alitii sheria na kabla ya maelezo zaidi kutoka kwa askari huyo feki wa usalama barabarani, mkuu huyo alijitambulisha kwa askari huyo.
Askari huyo wa Kituo cha Stakishari alisema: “Inapotokea askari mwenye cheo cha juu anapojitambulisha pengine kwa kuwa hukumfahamu kabla, kinachofuata ni saluti kabla ya kumruhusu kuendelea na safari lakini kitu hicho hakikufanyika hali ambayo ilimfanya bosi huyo akasirike.
Kinaeleza chanzo hicho kuwa askari waliotumwa kumfuatilia walipofika eneo hilo kwa ajili ya kumtambua na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kosa alilofanya, waliposimamisha gari na kumuita alitimua mbio kabla ya kutiwa mbaroni na kujifanya amepoteza fahamu mara baada ya kumdaka.
Askari hao walimbeba na kumpandisha  katika gari ‘defender’ hadi Kituo cha Polisi Stakishari ambako amefunguliwa jalada la kujifanya askari wa usalama barabarani akijua kuwa si kweli na atafikishwa mahakamani leo kujibu mashtaka yanayomkabili.
Maelezo yake Polisi
Askari huyo bandia ambaye amefunguliwa jalada namba STK/RB/15305/2013, amedai katika maelezo yake kuwa kamba ya filimbi na kizibao ni vya polisi isipokuwa vifungo cha kung’ara  havikuwa vya polisi .
Askari huyo alidai kuwa nguo nyeupe juu ya kofia aliitengeneza kienyeji, wakati krauni, tepe za usajenti na mkanda ni vya shemeji yake ambaye alikuwa polisi mkoani Tabora ambaye alimtaja kwa jina moja la Shaaban. Mtuhumiwa huyo anasema katika maelezo yake hayo kuwa alijiunga na Chuo cha Polisi Moshi mwaka 1990 kabla ya kutimuliwa mwaka uliofuata kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu na alikuja mjini hivi karibuni baada ya kufiwa na mtoto na mkewe na maisha kuwa magumu huko Tabora.
Habari zaidi zinaeleza kuwa katika sare za trafiki alizokutwa , ndani alivaa na nguo nyingine za kiraia ndani na inadhaniwa kuwa huwa anaziweka nguo hizo katika mfuko na kuzivaa akifika eneo la jirani na hapo alipoamua kuwa kituo chake cha kazi kuzivua hizo za trafiki baada ya kukamilisha siku.

No comments:

Post a Comment