Wednesday, 21 August 2013

KLABU ya Yanga, kati ya leo na kesho inatarajiwa kukata rufaa kupinga adhabu aliyopewa mshambuliaji wake, Mrisho Ngasa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Wiki iliyopita, kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa, ilimwadhibu Ngasa, kifungo cha mechi sita na kulipa sh milioni 45 kwa klabu ya Simba, kutokana na kusaini mkataba kabla ya kwenda Yanga.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, alisema jana kuwa wanatarajia kuwasilisha pingamizi TFF, ambayo itakuwa na mambo matatu muhimu, kwani barua waliyoipata kutoka Shirikisho hilo haijaeleza kwa undani mambo hayo.
Mwalusako alisema, kwanza, watahoji endapo kamati imebariki Ngasa ni halali Yanga, iweje wamfungie mechi sita? Pili, barua waliyopewa haina sehemu inayoonesha mchezaji huyo alisajiliwa na Simba na tatu, haijaonesha vipengele vya kanuni vilivyotumika kutoa adhabu hizo.
Kwa mujibu wa Kamati ya Mgongolwa, endapo Ngasa atashindwa kulipa fedha hizo ndani ya mechi sita alizofungiwa, ataendelea kusota benchi hadi atakapotekeleza adhabu hiyo.

No comments:

Post a Comment