Thursday 22 August 2013

Watanzania zaidi ya 100 wako gerezani nchini China kuhusiana na dawa za kulevya, 20 ni wanawake!

Kama kuna jambo ambalo linaichafua Tanzania katika jukwaa la kimataifa kwa siku hizi, basi ni tatizo la usafirishaji wa dawa za kulevya.
Zamani tatizo hili halikuwa kubwa sana, ni mtanzania mmoja mmoja sana alikuwa akikamatwa nje kwa kusafirisha dawa za kulevya. Kwa hiyo jina la nchi yetu lilikuwa linasikika mara moja moja sana au kwa bahati mbaya kuhusiana na tatizo la dawa za kulevya. Lakini katika siku za hivi karibuni tumesikia kuwa kuna watanzania wanakamatwa Ulaya, Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, Asia na hata katika nchi za Afrika, kama ilivyotokea majuzi huko Afrika Kusini. Kwa sasa ukisikia jina la Tanzania linatajwa kuhusiana na tatizo la dawa za kulevya, si bahati mbaya tena na si mara moja moja kama zamani.
Serikali yetu imekuwa ikijitahidi sana kujenga jina zuri la Tanzania na kuitanganza Tanzania kuwa ni kisiwa cha amani, nchi yenye vivutio vingi vya utalii na yenye ukarimu kwa wageni. Na kweli kama ukitembelea nchi yoyote yenye watu wanaoifahamu Tanzania, si vigumu kusikia Tanzania ikisifiwa, lakini kama ukiona mtu amekaa kimya, basi ujue kuna uwezekano kuwa hataki kutaja suala la dawa za kulevya.
Mwanzoni nilikuwa naamini kuwa watanzania ni watu wenye maadili ambao wanapokwenda nje ya nchi wanakumbuka kuwa “mabalozi wazuri” wa nchi. Lakini baada ya kutembelea sehemu mbalimbali duniani, hasa nchi za Asia na Asia Kusini Mashariki, na kukutana na wenyeji na kuwauliuza mtazamo wao kuhusu Tanzania na watanzania, nikagundua kuwa sifa zote nzuri za Tanzania zinafunikwa na sifa mbaya moja au mbili. Kubwa ni tatizo la dawa za kulevya, na nyingine ni ukahaba (Hong Kong).
Pamoja na kuwa ni watanzania wachache sana wanaosafirisha dawa za kulevya, ni hao wachache ndio wanaofanya jina la watanzania wengine walio wengi lichafuke, na kuwafanya watanzania wanaokwenda nje ya Tanzania kwa malengo halali, kama vile biashara, michezo na hata utalii, wakumbwe na matatizo wasiyostahili.
Zamani nilikuwa ninakasirika sana ninapotolewa kwenye mstari wa uwanja wa ndege na kuanza kupekuliwa na kuulizwa maswali ‘ya kipuuzi’, kana kwamba mimi ni mhalifu au mtuhumiwa wa uhalifu. Nilikuwa najihisi kuwa mimi ni mhanga wa ubaguzi wa rangi, kitu ambacho sikutegemea kutoka kwa nchi marafiki zetu. Kuna wakati hata nilifikia hatua ya kukwaruzana na maofisa wa uwanja wa ndege, kwa kuona wananitendea isivyostahili. Lakini baadaye baada ya kuangalia hali halisi na kuona matendo yanayofanywa na baadhi ya watanzania wanaokuwa nje ya Tanzania, nikagundua kuwa wasiwasi walionao maofisa wa viwanja vya ndege vya nchi za Asia kuhusu watu wenye pasi za kusafiria za Tanzania, ni wa haki na unaeleweka, si ubaguzi wa rangi na si ubaguzi dhidi ya watanzania. Kama ni ubaguzi wa rangi, basi matendo ya baadhi yetu ndio yanawapa kisingizio cha kufanya hivyo.
Kinachonifanya nisione kuwa ni ubaguzi wa rangi ni kuwa, nchini China kwa mfano kuna adhabu kali sana kwa watu wanaokamatwa kwa makosa ya dawa za kulevya, wachina wengi wamehukumiwa adhabu ya kifo. Lakini cha ajabu ni kuwa watanzania wanaokamatwa kwa makosa sawasawa na wanayofanya wachina, wanapewa vifungo virefu na adhabu ya kifo, lakini hadi sasa hakuna mtanzania aliyenyongwa ikilinganishwa na wachina na wafungwa wa mataifa mengine.
Kumekuwa na habari za kupotosha kwenye baadhi ya vyombo vya habari vya Tanzania kuhusu jambo hili, lakini ukweli ni kuwa Mpaka sasa hakuna mtanzania aliyehukumiwa adhabu ya kifo kwa makosa ya dawa za kulevya na adhabu yake kutekelezwa. Ni vigumu kujua ni kwanini China haijawanyonga watanzania, lakini ukiangalia sababu ya wachina kutowachukulia hatua kali watanzania, utaona kuwa wanathamini sana urafiki uliojengwa na viongozi wetu, hasa mwalimu Nyerere na mzee Salim Ahmed Salim. Kwa hiyo ukiona jinsi wenyeji wanavyochukuliwa hatua kali, na sisi watanzania “kudekezwa”, hata ukikutana na vitendo vinavyokukosesha raha unapopita uwanja wa ndege, basi inabidi uwe mpole mara moja.
Pamoja na kuwa kila suala la dawa za kulevya linapotajwa, utakachoona kwenye vyombo vya habari ni kuwa kuna mtandao mkubwa wa siri, lakini ni kama tunapuuza madhara yanayoletwa na jambo hili kwa uhusiano kati ya nchi yetu na nchi nyingine, na usumbufu linaoleta kwa watanzania wengine wasio wasafirishaji wa dawa za kulevya.
Inasikitisha kuona kuwa kati ya watu kutoka nchi za Afrika Mashariki, ni watanzania ndio wanaokamatwa zaidi na dawa za kulevya kuliko wale wakenya na waganda. Na hata watanzania wanaokamatwa, wengi wanatoka katika Mikoa miwili ya pwani, ambako baadhi ya vijana wanaona ni “ujiko” kusafirisha dawa za kulevya. Ukiongea na vijana hao, unaweza kuona kuwa hawana elimu hata kidogo, kwani hata uwezo wao wa kuandika kwa Kiswahili na uwezo wa kuongea Kiswahili na kujenga hoja ni mdogo sana, ndio maana inaonekana ni rahisi kwao kurubuniwa kuliko vijana wa Kenya, Uganda na wa nchi nyingine za Afrika Mashariki. Wengi wao wanasema wanaahidiwa kati ya dola elfu mbili na elfu nne wakifikisha “mzigo” salama. Kwa kweli hizo si pesa nyingi ikilinganishwa na hatari ya kazi yenyewe, na hasa ukizingatia kuwa kwa mtanzania anayejituma kufanya kazi nyumbani, anaweza kupata pesa hizo.
Kwa hapa China, mpaka sasa naweza kusema kwa sasa tatizo limefikia kiwango cha kutia hofu, na hasa kwa Hong Kong na Makau ambako kuna wafungwa zaidi ya 100 wa kitanzania. Tofauti na siku za nyuma, idadi ya wafungwa wa kike inazidi kuongezeka siku hadi siku ambapo kwa sasa kuna wafungwa wa kike zaidi ya 20 katika magereza ya China bara na Hong Kong. Kutokana na hali hiyo nina wasiwasi kuwa huenda ile hadhi ya watanzania kuingia katika miji hiyo bila Visa huenda iko mashakani. Lakini vigumu kwangu kama mwandishi wa habari kujua undani wa tatizo hili. Ninachojua ni kuwa kuna watanzania wengi wako gerezani, kutokana na kukamatwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.
Niliwahi kumuuliza aliyekuwa balozi wa Tanzania hapa China na balozi wa sasa kuhusu athari ya tatizo hili kwenye uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania, wote walioonesha kukasirishwa na kusikitishwa na jambo hilo, na kusema linatia aibu. Lakini mabalozi hao hawajui ni nani anayewatuma watanzania wanaokamatwa na dawa za kulevya. Waliokamatwa nao hata siku moja hawataji ni nani aliyewatuma, wao ni kama watu waliokula yamini ya kutosema lolote, hata kama wanapewa adhabu ya kifo. Hata hivyo, wafungwa wanaeleza tu kwamba “Kuna mtandao mkubwa ambao unahitaji ushirikiano mkubwa kupambana nao, zinakopelekwa na zinakotoka dawa hizo”.
Hivi karibuni tumesikia alichokifanya Dk Mwakyembe kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, yeye anaona kuwa uwanja unaobeba jina la Mwalimu Nyerere haupaswi kuhusishwa na dawa za kulevya. Alichofanya Dk Mwakyembe pale uwanja wa ndege kwa kweli ni jambo zuri, na kama asingefanya hivyo huenda watanzania tungeendelea kuwa kizani kuhusiana na mambo yanayoweza kuwa yanaendelea katika forodha zetu. Lakini tukiangalia kwa undani tunaweza kuona kuwa, kama uhalifu huo unatokea kwenye uwanja wa ndege unaotakiwa kuwa na usalama mkali, hali ikoje kwenye forodha nyingine mbali na ile ya uwanja wa ndege wa mwalimu Nyerere ambako hakuna kamera za video, ambako Dk Mwakyembe hawezi kwenda kwa ghafla? Kuna Namanga, Holili, Horohoro, Silari, Tunduma nk, hali ya huko ikoje? Dk Mwakyembe anatakiwa kuhakikisha kuwa kilichofanyika katika Uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere kifanyike katika forodha zote. Dk Mwakyembe analia na jina la Mwalimu Nyerere, lakini ni vizuri watanzania wote tukikumbuka kuwa tunatakiwa kulia na jina la nchi yetu, Tanzania.
Kama hali hii ikiendelea inaweza kufika hatua kuwa wanafunzi, wafanyabiashara, wanamichezo, wagonjwa na hata watalii kutoka Tanzania wanaokwenda nje ya nchi, wote watawekwa kwenye kundi la washukiwa wa biashara ya dawa za kulevya.
- See more at: http://www.fikrapevu.com/watanzania-zaidi-ya-100-wako-gerezani-nchini-china-kuhusiana-na

No comments:

Post a Comment