SIKU chache baada ya kurejea Yanga, mshambuliaji Hamis Kiiza amepata timu inayotaka aende nchini Lebanon kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa.
Uongozi wa Yanga umeonyesha uko tayari kumuachia iwapo kila kitu kitakwenda vizuri na kufuata utaratibu unaotakiwa.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Bin Kleb, ambaye hushughulikia masuala ya usajili ya Yanga, amesema tayari wameshaijibu barua iliyoandikwa na timu hiyo ya Lebanon inayomhitaji straika huyo.
“Tayari uongozi unashughulika na suala hilo na umeihoji timu hiyo kama kweli inamtaka Kiiza kwa ajili ya majaribio au kumnunua. Maana kidogo barua yao hatujaielewa vizuri,” alisema Bin Kleb.
“Uongozi wa Yanga hautakuwa na kinyongo kumuachia Kiiza kama klabu hiyo itatoa ofa nzuri lakini pia tutazungumza na mchezaji mwenyewe kama atakubali, basi tutafanya hivyo.”
Kiiza ameanza mazoezi ndani ya siku chache tu akiwa amerejea nchini akitokea Uganda baada ya kutaka apewe dau la dola 50,000 (Sh milioni 81). Hata hivyo uongozi wa Yanga ulimpa dau la dola 35,000 (Sh milioni 57).
Tayari Kiiza ameanza mazoezi na kikosi cha Yanga chini ya Brandts, hata hivyo amekuwa akionekana hayupo fiti, jambo linaloashiria hakuwa akifanya mazoezi.
No comments:
Post a Comment