Wednesday 21 August 2013

Chelsea yapata ushindi wenye utata.


Bao la kipindi cha pili lililofungwa na Branislav Ivanovic kwa kichwa ndilo lililoamua hatima ya Chelsea jumatano usiku kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Stamford Bridge.

Chelsea walianza kwa kufunga kwa shuti la Eden Hazard ambalo lilisindikizwa golini na Antonio Luna wakati akijaribu kuokoa.Lakini Christian Benteke aliisawazishia Villa kwa bao zuri.
Licha ya ushindi huo kwa Chelsea mechi hiyo iligubikwa na utata kutokana na maamuzi ya mwamuzi wa kati Kevin Friend.
Tukio kubwa ambalo limetawala na kuibua utata ni pale beki wa Chelsea Ivanovic alipopewa kadi ya njano kwa kosa la kumpiga au kutishia kumpiga usoni mshambuliaji wa Villa, Christian Benteke.
Kitendo hicho kimesemwa kuwa kilistahili kadi nyekundu badala ya njano aliyopewa Ivanovic, japo kocha wa Chelsea Jose Mourinho amesema kadi hiyo ya njano ilikuwa ni adhabu tosha kwa mchezaji wake.
Kocha wa Aston Villa Paul Lambert ameilalamikia maamuzi ya mechi hiyo ikiwemo pia penati ambayo walinyimwa Villa baada ya John Terry kuushika mpira kwenye eneo la hatari.
Hata hivyo Mourinho amekiri haikuwa mechi rahisi kwake, na kusema "hiki ndicho nimekuwa nikikosa nilipokuwa Hispania,pale kila mechi tunashinda tukiwa nyumbani bila wasiwasi wowote,lakini hapa England mambo ni magumu,uwe nyumbani au ugenini."
Mourinho hajawahi kufungwa kwenye uwanja wa Stamford Bridge,kwani ana rekodi ya kushinda michezo 48 na kutoka sare 14 katika michezo 68 aliyoingoza Chelsea tangu alipofika mara ya kwanza.
Jumatatu Mourinho atakuwa na kibarua kigumu mbele ya Manchester United kwenye uwanja wa Old Traford, kabla ya kwenda kupambana na Bayern Munich katika mechi ya kombe la mabingwa wa Ulaya maarufu kama Super Cup.

No comments:

Post a Comment