Sunday 18 August 2013

CHADEMA yafukuza wanachama wake nane


KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Ukonga imewafukuza uanachama wanachama wake wanane huku wawili wakipewa onyo kali kwa tuhuma za kukihujumu.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa CHADEMA Jimbo la Ukonga, Jumaa Mwipopo, alisema kuwa kwa muda mrefu kulikuwa na tuhuma za wanachama hao kukihujumu chama hicho kwa kufanya vikao vya siri ili kuwarubuni wanachama na viongozi wa matawi kukihama.
Mwipopo alisema kuwa mikakati hiyo ilikuwa ikiratibiwa na Mchungaji Zabron Shilinde na Habibu Rajabu.
Alisema kuwa Mchungaji Shilinde awali alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Kitunda, lakini alivuliwa uongozi Aprili 10, 2012 kutokana na tuhuma mbalimbali, ikiwamo kuchukua fedha za chama na kuzitumia bila idhini na kuchukua kadi za chama kwenye kata na matawi bila kujulikana alikokuwa akizipeleka, tuhuma ambazo alikiri, hivyo kubaki kuwa mwanachama wa kawaida.
Akimzungumzia Rajabu, Mwipopo alisema kabla ya kufukuzwa uanachama alikuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Kata ya Kitunda.
Aidha, Katibu huyo wa Jimbo la Ukonga alisema kuwa tuhuma zinazowakabili Shilinde, Rajabu na wenzao sita ni kupokea fedha kutoka kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduazi (CCM) ili zitumike kuwashawishi viongozi na wanachama wa matawi mbalimbali wa chama hicho kujiondoa CHADEMA na kujiunga na CCM.
Mwipopo aliwataja watuhumiwa wengine waliofukuzwa uanachama tangu Agosti, 15, 2013 ni Joshua Kisoko - Mwenyekiti wa Tawi la Msingi Masesko, Esther Joshua Kisoko - Katibu wa Kina Mama Kata ya Majohe, S. Ngazonga – mwanachama, J. Shomary - mwanachama, Pili Said – mwanachama na Surema Amali- mwanachama.
Vilevile aliwataja waliopewa onyo kali kuwa ni Lukasi Matindiko na Juma Ununzi, ambaye ni Mwenyekiti wa Tawi la Kwa Mpemba.
Mwipopo alibainisha kuwa: “Baada ya Kamati ya Utendaji kujiridhisha na ushahidi uliotolewa pamoja na kupitia mawasiliano yao, kutokana mkakati wao wa kushawishi wanachama na viongozi wa CHADEMA kukihama chama, kuanzia Agosti 15, 2013 si wanachama wetu tena na hawatakiwi kujihusisha na shughuli za chama.”

Chanzo Tanzania Daima.

No comments:

Post a Comment