Miaka ya hivi karibuni, kumeibuka wimbi kubwa la wanawake kwa wanaume ambao wanafanyia matengenezo maumbile yao ‘Plastic Surgery’ kama sura, kupunguza vitambi, kuongeza makalio, kuongeza au kupunguza matiti.
Awali wimbi hili lilibuka zaidi kwenye nchi za magharibi, lakini kutokana na utandawazi, dunia kuwa kijiji, kwa hivi sasa watu wengi wamekuwa na mwamko wa kutengeneza shepu katika sehemu mbalimbali za maumbile yao.
Kwa hapa Tanzania, watu wengi hukimbilia nchini India kwenda kufanya upasuaji wa aina hii ambao wengi wao wanafanya aidha kwa kujua au kwa kutokujua madhara yake, lakini lengo kuu ni kujipendezesha na kuonekana mwenye mvuto machoni mwa watu.
Dk Zaituni Sanya bingwa wa upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili alifanya mahojiano maalum na Mwandishi wa habari hizi na kusema: “Kwa hapa Tanzania upasuaji unaofanyika ni ule wa kurekebisha sura na ule wa matiti ndiyo sana.”alisema
Akifafanua zaidi alisema: “Kwa upande wa sura upasuaji tunaofanya ni kwa wale ambao utakuta wameota vinyama au wana uvimbe uvimbe kwenye sura, ndiyo tunawafanyia na tena upasuaji wake unatumia nyuzi nyembamba sana maalumu ambazo hazionekani, lakini ule wa kuchonga sura kama ule uliokuwa ukifanywa na kina Michael Jackson hatufanyi.
“Upasuaji wa matiti ndiyo tunafanya sana hapa nchini, mimi binafsi ninafanya na kwa hapa Muhimbili gharama zake ni zilezile kama za upasuaji mwingine wowote, lakini kwenye hospitali za binafsi upasuaji huu ni gharama sana.
“Wengi wanaokuja hapa unakuta niwasichana kuanzia umri wa miaka 20 hadi 35 na hawa wanakuja siyo kwamba wanaumwa la hasha, wanafanya upasuaji huu kwa ajili ya urembo tu, unakuta matiti yao ni makubwa hivyo wanakuja kwa lengo la kuyapunguza.
“Matiti makubwa yanasababishwa na chembe chembe ambazo zinatengeneza mafuta na kuyafanya kuwa makubwa kupita kiasi, tunapofanya upasuaji tunaondoa mafuta yaliyozidi na kuliweka titi kwenye umbo zuri ambalo mhusika atataka na kwa saizi ambayo atapendelea, na pia wakati wa kushona inabidi uangalifu sana ili isisababishe madhara.
Mbali na kupunguza wanaongeza?
“Kwa hapa Tanzania hapana, toka nimeingia kwenye udaktari wa upasuaji mwaka 2004 sijapata mgonjwa ambaye anahitaji kuongeza ukubwa wa matiti zaidi ni kuyapunguza, na hii si tu kwa hapa Muhimbili bali pia kwenye hospitali kubwa zote za watu binafsi hakuna wagonjwa wa aina hii zaidi ya wale wanaohitaji kupunguza.
Hata hivyo Dk Sanya alisema kuwa hana takwimu sahihi za idadi ya watu ambao wanaenda kwa ajili ya tatizo hilo zaidi ya umri ambao wengi wao ni wasichana kati ya miaka 20 hadi 35.
“Upasuaji wa kupunguza matiti hauna madhara yoyote kwa vile tunapunguza chembe chembe zilizozidi pamoja na mafuta na hatutumii kemikali zozote. Ila kama upasuaji wake utakosewa basi madhara ambayo muhusika atapata ni kuwa hatoweza kumnyonyesha mtoto na kama mnavyojua matiti yakijaa misuli inapanuka na hivyo ni lazima mhusika atapata maumivu makali ambayo yatatibiwa na dawa za kutuliza maumivu.“Kansa ni ugonjwa unaotokea tu kutokana na mfumo wa maisha na vyakula tunavyokula, lakini upasuaji huu wa kupunguza matiti hausababishi kansa, na maziwa mtoto asiponyonya kwa siku kadhaa ‘automatic’ yatakauka yenyewe ndiyo maana hata mama anayenyonyesha akiacha kumnyonyesha mtoto kwa wiki moja, mbili maziwa yanakauka.
“Ila kwa wale wanaongeza ukubwa wa matiti kuna madhara makubwa na si maziwa tu hata wale wanaongeza hipsi na makalio kwa kuwa ufanyaji wake unatumia kemikali... “Kitu chochote ambacho ni ‘artificial’ kina madhara na madhara makubwa ya kemikali zinazotumika kuongeza maziwa, hipsi na makalio ni saratani kwa kuwa ngozi ni ‘delicate’.
“Watu wanaofanya upasuaji huu kwa ajili ya urembo lazima watakuwa wanatumia maisha yao yote (medication) hali hii ni kujilimbikizia dawa mwilini, mwisho wa siku anajiua mwenyewe kama ilivyotokea kwa Michael Jackson.
No comments:
Post a Comment