Wednesday, 21 August 2013

Yanga yaburuzwa TFF,NSAJIGWA, MWASIKA WAIKABA KOO

KLABU ya Yanga imeburuzwa kwa mara nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutokana na kushindwa kuwalipa nyota wake wawili wa zamani deni la sh milioni 16.
Wachezaji walioishtaki Yanga TFF ni aliyekuwa nahodha wake muda mrefu, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, ambaye hivi sasa ni Kocha Mkuu wa Lipuli ya Iringa na Stephano Mwasika, aliyeko Ruvu Shooting ya Pwani.
Hii itakuwa si mara ya kwanza Yanga kushtakiwa katika vyombo vya juu vya soka na hata mahakamani, kutokana na kushindwa kuwalipa wachezaji na wafanyakazi wake inaoachana nao.
Baadhi yao ni Mkenya, John Njoroge, Kocha Kostadin Papic, Steven Marashi, Mmalawi Wisdom Ndlovu, aliyekuwa Ofisa Habari, Louis Sendeu na Katibu Mkuu, Celestine Mwesiga.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, katika kuonekana kujihami na sakata hilo, alikiri kudaiwa deni hilo linalotokana na ada ya usajili na kuwa, waliwaita Fuso na Mwasika ili walizungumze hilo juzi, lakini hawakutokea na wala simu zao za viganjani hazikupatikana.
Mwalusako alisema wamesikia tetesi za wachezaji hao kwenda TFF kuwashtaki, wakati suala hilo liko mezani na mikataba yao inasema mchezaji anaweza kulipwa kidogo kidogo hadi deni lake kumalizika.
“Nimeamua kuwaita hapa kuzungumzia suala moja la Mwasika na Nsajigwa, tumesikia wamekwenda kutushtaki TFF, na sisi tuliwaita ili tuzungumze na kumalizana lakini hawakutokea, tumeona tuwaambie yasije yakafika kwenu mkaandika,” alisema Mwalusako na kuongeza kuwa, Nsajigwa anadai sh milioni 10 na Mwasika sh milioni sita.
Tanzania Daima iliwasaka Mwasika na Nsajigwa kuzungumzia suala hilo ambao walikiri kwenda TFF, baada ya kuona uongozi wa Yanga unawazungusha juu ya madai yao ambayo ni halali, baada ya kumaliza mikataba yao.
Mwasika alisema wao si watoto wadogo hadi waamue kwenda TFF bila sababu muhimu na kuwa kilichosababisha kupiga hodi vyombo vya juu ni ili kupata msaada wa kulipwa fedha zao ambazo walitakiwa kuzipata kabla hata ya kumaliza mikataba yao.
Alikwenda mbali na kudai kuwa, Mwalusako anaudanganya umma, kwani licha ya kutakiwa kuwalipa fedha zao Januari mwaka huu, hajawahi kuwaita kwa ajili ya mazungumzo na hiyo ni kutaka kujitetea.
Alihoji, hivi sasa yeye si mchezaji wa Yanga, yuko Ruvu Shooting, atawezaje kuacha kazi yake na kwenda Yanga kujadili mambo hayo?
“Dada yangu kwanza mimi nakushukuru kwa kunipigia simu, kwa sasa nawaza nifanyeje ndani ya timu yangu ya Ruvu Shooting na mimi nawadai Yanga, wanilipe changu tumalizane, hawajatuita kuzungumza nao kama wanavyodai, kila siku wanatuzungusha, ndiyo maana tumeamua kwenda TFF.
Huyo Mwalusako ni muongo, mimi nadai hela zangu na kama angeniita nikafuate ningekataa saa ngapi? Nawadai sh milioni 6.5 na si sita kama alivyosema,” alisema Mwasika.
Kwa upande wake Nsajigwa, alisema kwa sasa yeye yuko Iringa kikazi, muda wa kukaa na Yanga kuzungumzia stahiki zake hana, kwani cha muhimu sasa ni TFF kuwasaidia kutoa uamuzi na endapo itashindikana, wako tayari kwenda Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
“Mpaka kufikia hatua hii tumewavumilia sana na sasa tumechoka, ila tuna imani TFF watatusaidia na tunashukuru kama wao Yanga wamekubali kuwa tunawadai, hilo ndilo la msingi na mimi niko ‘bize’ na kazi zangu, siwezi kuacha kazi zangu nikaja Dar es Salaam kujadili mambo ya hela, tumechoka na hatukutaka kufikia hapa ila imebidi, kwani sisi si wachezaji wa kwanza kulalamika,” alisema Nsajigwa.

Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment