Sunday, 18 August 2013

Madiwani CCM kutua CHADEMA


MADIWANI wanane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Kagera waliofukuzwa uanachama wiki iliyopita wamekaribishwa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ndiye aliyewakaribisha madiwani hao wanaosubiri kufukuzwa rasmi na vikao vya Kamati Kuu ya CCM, vinavyotarajiwa kufanyika wiki hii mkoani Dodoma.
Madiwani waliofukuzwa na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni naibu meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).
Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Uhuru wa Bukoba Mjini, Mbowe alisema CCM imewachakachua madiwani hao wanane na hata wakibaki huko chama chao hakitawaona wa maana, kwa sababu chama hicho kinalea ufisadi.
Mbowe alisema CHADEMA wako tayari kuwapokea madiwani hao waliofukuzwa na kuwafundisha siasa za mageuzi.
“Tutasimama nao katika kujenga Bukoba mpya isiyo na ufisadi kama unaofanywa na Meya wa manispaa hiyo iwapo wataamua kuja kwetu, milango ipo wazi nawakaribisha,” alisema.
Mbowe alisema CHADEMA kinamuunga mkono Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Hamis Kagasheki (CCM), anayepinga ufisadi unaofanywa na meya kutoka chama chake, Anatory Amani.
Alisema CHADEMA itashirikiana na kiongozi yeyote kutoka CCM atakayekuwa tayari kupambana na ufisadi ulioshamiri kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.
“CHADEMA katika mambo ya ufisadi ina msimamno unaoeleweka na kwamba katika kupinga ufisadi kipo tayari kumuunga mkono yeyote bila kujali itikadi,” alisema Mbowe na kusisitiza kwamba hata kama meya angekuwa mwanachama wa CHADEMA kingeunga mkono afukuzwe.
“Hatuna masilahi ya kisiasa na Kagasheki lakini katika suala hili tunamuunga mkono. Nawapongeza madiwani wetu wa CHADEMA walioungana na mbunge huyo kupinga ufisadi wa meya na kusimamia masilahi ya wananchi wa Bukoba Mjini,” alisema Mbowe.
Mbowe aliikejeli CCM kuwa haiwezi kuwafukuza madiwani hao kwa sababu itakuwa imejimaliza na hawana uhakika wa kuzirejesha kata hizo ukiitishwa uchaguzi.
Alisema kutokana na hofu hiyo Makao Makuu ya CCM yaliamua kuwarejesha madiwani hao wanane waliofukuzwa na CCM Mkoa wa Kagera.
“CCM wanataka kutuiga CHADEMA tulivyofanya Arusha ambapo tuliwafukuza madiwani wanne na baadaye tulishinda kwenye uchaguzi mdogo. Nawaambia jaribuni kuwafukuza wa kwenu muone moto,” alisema.
Katika ziara hiyo aliambatana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, Mkurugenzi wa Sheria na Katiba, Tundu Lissu na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Magharibi, Dk. Rodrick Kabangila, ambao anashirikiana nao katika kukusanya maoni ya rasimu ya Katiba.
Mbowe na msafara wake walifanya mikutano mitano katika wilaya za Ngara, Kyerwa, Karagwe, Missenyi na Bukoba Mjini. Leo Jumapili watafanya mkutano katika Wilaya ya Muleba kabla ya kuelekea Kigoma.
Katika mkutano wa Karagwe, Mbowe alimpokea aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Karagwe/Kyerwa aliyehamia CHADEMA jana.
CCM wasigana
Mara baada ya CCM Mkoa wa Kagera kuwafukuza madiwani hao wanaodaiwa kuungana na upinzani kutaka kumng’oa meya wa CCM, Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kikao hicho hakina uamuzi wa mwisho.
Nape aliwataka madiwani hao kuendelea na kazi kwakuwa ni halali mpaka pale suala lao litakapojadiliwa na vikao vya Kamati Kuu.
Kauli hiyo ilipingwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Constancia Buhiye, ambaye alisema hatambui kauli ya Nape na madiwani hao walikwisha kufukuzwa.
Buhiye alisema msimamo wa CCM ni kwamba waliofukuzwa wamefukuzwa, si madiwani tena.

No comments:

Post a Comment