Dar es Salaam. Serikali imesalimu amri kwa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans na imeanza mchakato wa kuwezesha kuondolewa mahakamani, kesi ya muda mrefu baina ya pande hizo mbili, gazeti hili limebaini.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zinasema hatua hiyo ya Serikali inatokana na ushauri ambao imekuwa ikipewa na wanasheria wake kwamba “uwezekano wa kushinda kesi hiyo ni mdogo sana.”
Mvutano uliopo unatokana na Serikali kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC), ambayo iliipa ushindi Dowans Holdings ya Costa Rica katika kesi namba 15945/VRO.
Jana, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felichesmi Mramba kwa nyakati tofauti walisema Serikali ilikwishatangaza bungeni kwamba inakusudia kumaliza kesi zote ambazo zimekuwa zikizorotesha mipango ya maendeleo.
“Sifahamu kwa upande wa kisheria wamefikia wapi katika suala hilo (la Dowans), lakini niseme kwamba waziri wetu (Profesa Sospeter Muhongo), alitangaza bungeni kwamba lazima tuondokane na kesi ambazo zinatukwamisha, kwa hiyo kama wameanza majadiliano ni hatua nzuri,” alisema Maswi.
Maswi alisema baada ya Waziri Muhongo kutoa kauli hiyo bungeni, utekelezaji wake unapaswa kufanywa na wanasheria wa Serikali na kwamba mtu sahihi wa kuulizwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa sababu Tanesco ni shirika linalomilikiwa na umma kwa asilimia 100.
Kwa upande wake, Mramba alisema: “Ninachofahamu ni kwamba kuna maandalizi ya kuwezesha mazungumzo hayo kufanyika, kama ulisikiliza hotuba ya bajeti ya mheshimiwa waziri (Muhongo), alisema mpango wa Serikali ni kuondokana na kesi hizi.”
Awali, kulikuwa na taarifa kwamba Serikali imewalipa Dowans kiasi cha Dola za Marekani 78 milioni (Sh124.8 bilioni), lakini Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alikanusha taarifa hizo akisema hakuna ukweli kuhusu jambo hilo.
Akizungumza kwa simu kutoka Sudan jana, Dk Mgimwa alisema: “Kwa uelewa wangu hakuna malipo hayo, isipokuwa kwa masuala mengine ya kisheria unaweza kuwasiliana na AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali), nikirudi unaweza kupata taarifa zaidi.”
Hata hivyo, AG, Jaji Frederick Werema alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema Serikali haihusiki kwa namna yoyote na kesi ya Dowans na kwamba wanaopaswa kufahamu kwa undani suala hilo ni wale walioshtakiwa, akimaanisha Tanesco.
“Hiyo siyo kesi ya Serikali na haihusiki kwa namna yoyote ile, kaangalie parties (wahusika) zinazotajwa kwenye hati ya kiapo, hapo Serikali haipo bwana, kwa hiyo waulize wahusika wanaweza kuwa na information (taarifa) zaidi,” alisema Jaji Werema.
Suala la kufanyika kwa usuluhishi nje ya Mahakama pia nalo bado ni kitendawili kutokana na ukweli kwamba hata Kampuni ya Uwakili ya Rex Arttoneys ambayo imekuwa ikisimamia kesi Dowans hapa nchini, haifahamu kuwapo kwa mazungumzo hayo.Mmoja wa Mawakili wa Kampuni hiyo, Dk Thomas Nguluma alisema juzi kuwa hawafahamu chochote kuhusu mpango huo wa Serikali na kwamba ikiwa umeanza kufanyika basi wao hawakuhusishwa.
“Sisi bado tuna mkataba na Tanesco, lakini kwa hilo unalolisema kwa kweli kama lipo hatujahusishwa, kama tukihusishwa basi hatutakuwa na haja ya kuficha chochote,”alisema Dk Nguluma.
Kesi ya Dowans
Katika madai yao, Dowans walikuwa wakitaka walipwe kiasi cha Dola za Marekani 149 milioni kutokana na uzalishaji wa umeme na gharama za kukatishwa kwa mkataba wake, lakini ICC iliwapa tuzo ya kulipwa Dola za Marekani 65 milioni.
Wakati Dowans wakiwa kwenye mchakato wa kukazia hukumu hiyo katika Mahakama Kuu jijini London, Uingereza, Tanesco kupitia kwa mawakili wa Kampuni ya Matrix ya nchini humo waliwasilisha maombi ya kutaka kuahirishwa kwa ukaziaji huo, kutokana na kufunguliwa kwa kesi ya kuupinga katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Tangu wakati huo, Tanesco hawajawahi kushinda kesi yoyote kati ya tatu ambazo zimewahi kujitokeza katika shauri hilo, huku riba ya fedha wanazotakiwa kulipa kwa Dowans ikiwa watashindwa kesi, ikiongezeka kila kukicha.
Kutokana na kesi ambayo ilifunguliwa katika Mahakama Kuu na baadaye Mahakama ya Rufani hapa nchini, hivi sasa riba imesababisha fedha zinazopaswa kulipwa kwa Dowans kukaribia Dola 120 milioni (zaidi ya Sh190 bilioni).
Serikali kupitia Tanesco pia ililazimika kuweka dhamana ya Dola 31 milioni za Marekani (Sh50 bilioni) za dhamana kutokana na kesi zilizofunguliwa hapa nchini kuchelewesha kukaziwa kwa uamuzi wa ICC Uingereza.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment