Sunday 18 August 2013

Tindikali yauzwa kama njugu mitaani


Maeneo inakouzwa tindikali
Uchunguzi uliofanywa katika mitaa ya maeneo ya Vingunguti yenye viwanda vingi, umebaini kuwa kuna viwanda viwili vinavyouza tindikali na kwamba viwanda hivyo ndivyo vinavyotajwa kuwa wasambazaji wakubwa wa kemikali hiyo hatari hapa nchini.
Katika kiwanda cha kwanza mwandishi wetu alijifanya kuwa ni mteja anayehitaji kununua kemikali kwa ajili ya kutengeneza sabuni za mche, aliambiwa bei ya sulphuric acid ni Sh45,000 kwa lita 50 na Hydrogen Peroxide Sh60,000 kwa lita 30.
Muuzaji katika kiwanda hicho ambaye jina lake linahifadhiwa, alikiri kusikia agizo la serikali linalowataka kufuata sheria za uuzaji na usambazaji wa tindikali na kwamba baada ya miezi mitatu hawataruhusiwa kumuuzia mtu yeyote ambaye hatakuwa na leseni.
“Hata wewe tutakuuzia kwa sababu muda tuliopewa haujakwisha, lakini baada ya miezi mitatu hatutakuuzia haya madawa hadi uwe na kibali…hapa unaweza kupata mzigo kiasi chochote unachokihitaji hata lita 1,000,” alisema muuzaji huyo.
Katika kiwanda cha pili, ambacho kipo hatua chache kutoka kile cha kwanza, mwandishi wetu alijitambulisha getini kuwa ni mteja anayehitaji kununua kemikali kwa ajili ya kutengeneza sabuni za mche na maji.Muuzaji alichukua karatasi yenye orodha ya kemikali na bei zake kisha aliandika pembeni; sulphonic acid kilo10 Sh 35, 000 na Hydrogen Peroxide kilo 30 Sh53,100.
Hata hivyo, mwandishi wetu alinunua Sulphonic acid pekee yake na kukabidhiwa risiti (Tax Invoice) yenye kumbukumbu namba 129412 bila ya kupewa elimu ya tahadhari ya kuitumia.
Mtaalamu wa kemikali
Mtaalamu wa kemikali, Wiseborn Makaka, anasema kuwa kemikali za Hydrochroric acid, Sulphuric acid na Sulphonic acid zote zipo katika kundi moja lenye madhara makubwa kwa binadamu kulingana na wingi wa kemikali iliyotumika.
“Ukiwa umezinunua kama zilivyo yaani haujachanganya na maji, kitaalamu tunaita concentrated acid ni hatari sana. Iwapo utadondokewa hata na tone moja sehemu hiyo itaunguzwa na kuchimbwa kwa ndani, usipowahi kuosha kwa maji inaweza kuchimba hata mfupa ukaonekana,” anasema Makaka na kuongeza kuwa:
“Ukimwagiwa machoni unakuwa kipofu labda uoshe kwa maji mengi sana.”Mtaalamu huyo anaongeza kuwa kemikali hizo si rafiki wa nguo, kwani zikidondokea huiacha nguo ikiwa na matundu na kwamba mtu yeyote atakayekunywa tindikali atapoteza maisha yake.
“Ukiwekewa kwenye chakula huwezi kuishi, utakufa hii inatokana na kwamba mwili una protein, na protein ni amphoteric, hivyo endapo utakutana na acid tu lazima reaction itatokea,” anafafanua Makaka.
Vilevile, Makaka anasema kemikali za Hydrochloric acid na Nitric acid zina athari kubwa kwa binadamu iwapo atavuta hewa yake bila kuvaa kifaa cha usalama puani.
Anasema kwa ujumla kemikali zinazotumika kutengenezea sabuni za maji zimebainika kuwa na madhara makubwa zaidi zikilinganishwa na zile za mche.
Mtumiaji wa tindikali
Mkurugenzi wa Mode Integrated Solution, Mahmoud Omar ambaye kampuni yake inafundisha mafunzo ya kutengeneza sabuni na bidhaa nyingine anasema kuwa serikali inapaswa kutafakari upya uamuzi wake wa kudhibiti tindikali kwa kuwa utawaathiri wajasiriamali wengi wadogo.
Anasema wafanyabiashara wadogo wananufaika kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotumia tindikali, hivyo udhibiti uliowekwa na serikali utaifanya bidhaa hiyo kuuzwa kwa njia za panya. “Tamko la serikali linawaua wajasiriamali. Watu wengi tumewaokoa, sasa hivi kila mtu ana kiwanda kidogo nyumbani…kwa namna hii biashara itakuwa ya magendo,” anasema Omar.

No comments:

Post a Comment