Wednesday, 21 August 2013

Jairo, Nyoni watupwa

RAIS Jakaya Kikwete amewang’oa rasmi makatibu wakuu wawili waliokuwa wamesimamishwa kazi kutokana na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi zilizokuwa zikiwakabili katika wizara zao.
Makatibu hao ni David Jairo aliyekuwa Wizara ya Nishati na Madini na Blandina Nyoni wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Viongozi hao walisimamishwa kazi kwa vipindi tofauti mwaka juzi na mwaka jana ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao.
Jairo alisimamishwa kazi kwa tuhuma za kuandika barua kwa idara mbalimbali za Wizara ya Nishati na Madini na kuchangisha fedha ambazo zingetumika kuwashawishi wabunge wapitishe bajeti ya wizara yake kinyume cha utaratibu.
Nyoni alisimamishwa kazi pamoja na aliyekuwa mganga mkuu wa serikali, Dk. Deogratius Mtasiwa wakati mgomo wa madaktari wakidaiwa kuwa chanzo kutokana na kujihusisha na miradi ya kibishara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akitangaza mabadiliko hayo ya makatibu wakuu jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema uteuzi huo unalenga kuboresha utendaji serikalini.
Aliwataja walioteuliwa kuwa makatibu wakuu kwenye wizara nyingine ni Dk. Florence Turuka aliyekuwa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na sasa anakwenda Ofisi ya Waziri Mkuu.
Joyce Mapunjo kutoka Viwanda, Biashara na Masoko kwenda Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Alphayo Kadata aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Viwanda, Biashara na Masoko anakwenda Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wakati Shaaban Mwinjaka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Viwanda, Biashara na Masoko anakwenda Uchukuzi, Uledi Mussa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ushirikiano wa Afrika Mashariki anakwenda Viwanda, Biashara na Masoko.
Uteuzi huo pia umemgusa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) Sifuni Mchome anayekuwa Katibu Mkuu Elimu na Mafunzo ya Ufundi, huku Charles Pallangyo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anakuwa Katibu Mkuu Afya na Ustawi wa Jamii.
Waliopandishwa vyeo kutoka manaibu na kuwa makatibu kamili kwenye wizara hizo hizo ni Jumanne Sagini (Tamisemi), Servacius Likwelile (Fedha na Uchumi) na Patrick Makungu (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine ni Anna Maembe (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), Sihaba Nkinga (Habari, Vijana Utamaduni na Michezo) na Sophia Kaduma (Kilimo Chakula na Ushirika).
Awali Balozi Sefue alisema Rais Kikwete amemteua Dk. Donan Mmbando kuwa Mganga Mkuu wa Serikali akishika nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Mtasiwa aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi atakayeshughulikia afya.
Akifafanua sababu za uteuzi wa Dk. Mtasiwa, Balozi Sefue alisema: “Tuhuma zake hazikumfanya rais aamini kwamba anastahili adhabu ndiyo maana amempangia kazi nyingine.”
Kwa upande wa manaibu makatibu wakuu, walioteuliwa na waendako kwenye mabano ni Angelina Madete (Makamu wa Rais Mazingira), Regina Kikuli (Ofisi ya Waziri Mkuu), Zuberi Samataba na Edwin Kiliba (Tamisemi).
Wengine ni Dk. Yamungu Kayandabila (Kilimo, Chakula na Ushirika), Profesa Adolf Mkenda, Dorothy Mwanyika (Fedha na Uchumi), Rose Shellukindo (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Selassie Mayunga (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi).
Wamo pia Monica Mwamunyange (Uchukuzi), Consolata Mgimba (Elimu na Mafunzo ya Ufundi), Profesa Elisante Ole Gabriel (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) na Armatius Msole (Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
Balozi Sefue aliwataja manaibu makatibu waliohamishwa kuwa ni John Mngodo kutoka Uchukuzi kwenda Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Selestine Gesimba kutoka Elimu na Mafunzo kwenda Maliasili na Utalii.
Uhamisho huo umemgusa pia Injinia Ngosi Mwihgava kutoka Makamu wa Rais kwenda Nishati na Madini, Maria Bilia kutoka Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenda Viwanda na Biashara wakati Nuru Milao aliyekuwa Maliasili na Utalii akipelekwa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Watakaopangiwa kazi nyingine ni Sethi Kamuhanda aliyetoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamadini na Michezo, Kijakazi Mtengwa aliyekuwa Jamii, Jinsia na Watoto na Omari Chambo aliyekuwa Uchukuzi wakati Peniel Lyimo aliyekuwa Ofisi ya Waziri Mkuu akihamia Ikulu kama naibu mtendaji mkuu mwenye jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo.
Kwa mujibu wa Balozi Sefue, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi Patrick Rutabanzibwa amestaafu kwa hiyari.

Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment