Wednesday, 21 August 2013

Mwanasiasa wa Sweden ajeruhiwa Somalia

Watu waliokua na silaha wamewaua watu wawili na kumjeruhi mwanasiasa wa Sweden Ann-Margarethe Livh baada ya kushambulia gari lake mjini Mogadishu, Somalia.
Ann-Margarethe LivhMaafisa wanasema watatu hao walishambuliwa wakati wakirejea katika hoteli ya mwanasiasa huyo baada ya kutoa hotuba kuhusu demokrasia katika chuo kikuu mjini humo.
Hakuna kundi lililodai kutekeleza shambulio hilo wala sababu za kumlenga Bi Livh. Somalia inakabiliwa na maasi ya wanamgambo wa kiisilamu wa Al Shabaab ambapo pia inakumbwa na visa vya jinai.
Wiki jana shirika la misaada la Medecins Sans Frontier{MSF} lilitangaza kufunga huduma zake zote nchini Somalia kutokana na mashambulio dhidi ya wafanyikazi wake.
Somalia imekua bila serikali thabiti tangu kuondolewa madarakani kwa utawala wa Siad Barre mwaka wa 1991.
Duru za usalama zimesema Bi Livh amepokea matibabu katika hospitali ya wanajeshi wa Muungano wa Afrika mjini Mogadishu. Msemaji wa chama cha Ann-Mararethe Livh amesema mwanasiasa huyo alipata majeraha ya risasi.
Kwa sasa kuna mipango ya kumsafirisha hadi mjini Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi.Familia yake imesema mwanasiasa huyo alikua shwari licha ya majeraha.
Takriban wanajeshi 18,000 wa Muungano wa Afrika wanashika doria nchini Somalia ili kusaidia serikali mpya ya Somalia. Utawala wa sasa ndio wa kwanza kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, Marekani na Shirika la Fedha duniani kwa zaidi ya miongo miwili.
Wapiganaji wa Al Shabaab wameondolewa mjini Mogadishu lakini wanathibiti maeneo kadhaa ya Somalia. Kuna makundi mengine ya kikoo ambayo yanathibiti maeneo mengi ya Somalia.

No comments:

Post a Comment