Wednesday, 21 August 2013

Urais wamtesa Makamba, VYUO VIKUU WAKANA TAMKO LA KUMUUNGA MKONO

NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba amechafua hali ya hewa kwa viongozi wa vyuo vikuu, akidaiwa kuwatumia baadhi yao kujisafishia njia ya urais 2015.
Siri hiyo imefichuka zikiwa ni siku tano tangu Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe tawi la Mbeya, Theonest Theophil atoe taarifa akidai kuwa viongozi wa vyuo vikuu 21 nchini wameazimia kuunda timu ndogo kumshawishi awanie urais.
Katika tamko hilo ambalo limebatilishwa jana na Taasisi ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini (Tahliso), Theophil alisema maazimio hayo yalifikiwa katika mkutano wa siku mbili na  kuwashirikisha marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu na maspika wa vyuo 21 nchini.
Theophil alisema mkutano huo uliyapigia kura majina matatu ya wabunge vijana wakiwemo pia John Mnyika na Zitto Kabwe wa CHADEMA, na kwamba Makamba alipitishwa kuwa chaguo lao baada ya kupata kura 70 kati ya 105 zilizopigwa.
Kwamba Zitto alipata kura 20 na Mnyika kura tisa, huku kura tisa zikiharibika.
Hata hivyo, taarifa hiyo iliibua mvutano mkali baina ya viongozi wa vyuo mbalimbali wakisema kuwa semina hiyo haikuwa ya kujadili suala hilo na kwamba hakuna kura zilizopigwa.
Badala yake viongozi hao walidai kuwa taarifa hiyo ya upotoshaji iliandaliwa kwa makusudi na baadhi ya wenzao ambao wamekuwa wakijaribu kuitumia taasisi hiyo kwa malengo ya kumpigia chapuo Makamba ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli.
Wakati hali ikiwa hivyo, asasi isiyokuwa ya kiserikali inayojihusisha na mapambano dhidi ya maradhi, ujinga na umasikini (FDIP) ambayo iliitisha semina hiyo mkoani Morogoro, imekuwa na kauli za kugongana na mtoa taarifa za maazimio.
Katibu Mkuu wa FDIP, Francis Nduguru alipobanwa na gazeti hili jana, alidai kuwa aulizwe Theophil ambaye alitoa taarifa ya maazimio hayo ya semina ya siku mbili.
“Sitaki usumbufu, hao viongozi wanakulalamikia wewe kama nani? Waite walalamikie kisha tumia taaluma yako kufanya kile ambacho kinakusaidia, nimemaliza,” alisema Nduguru na kisha kukata simu.
Naye Theophil alipoulizwa alitoa tamko hilo kama nani wakati Tahliso wanalipinga, alirusha mpira akisema “naona vyema ungewauliza waandaji wa semina hiyo.”
Alipoelezwa kuwa nao wamemtaka alifafanue yeye, alikiri kuwa semina hiyo haikuwa ya Tahliso, lakini walikuwa wakijadili changamoto zinazowakabili vijana ikiwemo ya kukosa uwakilishi katika vyombo vya uamuzi.
“Alipoulizwa agenda ya kumchagua Makamba ilitoka wapi, alisema kuwa katika majadiliano jina la mbunge huyo lilitajwa na vijana wengi, lakini akataka waandaaji wa semina hiyo ndio watoe ufafanuzi.
Makamba hakupatikana kuzungumzia madai hayo kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa, na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi hakujibu.
Gazeti hili lilifanikiwa kupata nakala ya barua ya mwaliko na ratiba ya semina hiyo ambapo suala la wajumbe kujadili wagombea na kuwapigia kura halikuonyeshwa popote.
Rais wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Katoliki cha Afya na Tiba-Bugando (CUHAS-Bugando) Mwanza ambaye ni mmojawapo wa viongozi wanaopinga taarifa ya Makamba kupigiwa debe na vyuo, alisema kuwa wasomi wa vyuo vikuu hawawezi kufanya jambo ambalo ni kinyume na katiba za serikali zile za vyuo.
“Kiongozi wa serikali kusimama na kutoa tamko la kumuunga mkono mtu ambaye ni mwanachama wa chama fulani cha siasa kwa mujibu wa katiba za serikali zetu haturuhusiwi kwani si za vyama vya siasa,” alisema Moses Mdede.
Nayo Tahliso katika taarifa yake iliyosainiwa na Katibu Mkuu Mtendaji Donati Salla, ilieleza kusikitishwa na maazimio hayo kwa kuwa yalikuwa kinyume na maadili ya elimu ya juu nchini.
“Tahliso inasema mkutano huo wa Morogoro ni batili na hautambuliki kwa mujibu wa sheria Na 7 ya vyuo vikuu ya mwaka 2005,” alisema.
Salla aliongeza kuwa shughuli za wanafunzi wa vyuo vikuu vya elimu ya juu ni kushughulikia masuala ya wanafunzi na ubora wa taaluma itolewayo katika chuo husika na masuala mengineyo ya kitaifa yasiyokuwa ya kisiasa.
“Hatua zilizochukuliwa na Tahliso ni kuwaonya viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu ambao walishiriki mkutano huo wa Morogoro na kuwataka wasirudie tena kufanya hivyo,” alisema.
Vyanzo vyetu vya habari vinadai kuwa semina hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Uluguru, ilionekana wazi kuwa ilipangwa makusudi kumjenga kisiasa Makamba.
Kwa mujibu wa nyaraka tulizonazo, ajenda zilizojadiliwa ni elimu na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Katika hili vijana walitakiwa kutoa mawazo yao juu ya mfumo wa elimu nchini kwa ujumla na wachangiaji pia waligusia suala la mikopo ya wanafunzi.
Katika tatizo la ajira nchini hasa kwa vijana ambao wengi wao ni wahitimu wa vyuo vikuu, mada hii nayo ilijadiliwa kwa wachokoza mada na wajumbe kujadili na kutoka na mapendekezo.
Kuhusu vijana na siasa, ajenda hii ilijikita katika mrengo wa namna gani vijana wataweza kuhusika katika siasa ya nchi hasa katika chaguzi zijazo kuanzia serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu mwaka 2015.
“Kilichoonekana katika semina ile ni kwamba viongozi wa vyuo vikuu waliohudhuria walikuwa ni wachache sana na hawakufika idadi hiyo iliyotajwa na vyombo vya habari.
“Wajumbe wengi waliohudhuria walionekana ni watu waliokuwa wameandaliwa maalumu kwa ajili ya kazi fulani kwani kuna ambao walionekana hata hawakuwa wanachuo,” kilisema chanzo hicho.
Katika hatua ya kushangaza wakati semina inaanza mwenyekiti alikuwa tayari ameshaandaliwa kinyume cha utaratibu kwani mwenyekiti hupendekezwa na kuchaguliwa na wajumbe.
“Pia mfumo wa kujadili mada zilizochokozwa ulikuwa ni wa makundi. Katika kila kundi ilionekana kulikuwa na mamluki waliowekwa ili kufanikisha mpango huo.”
“Ilipofika katika mada ya vijana na siasa, kwenye kila kundi ilionekana kulikuwa na mtu aliyetaka wajumbe watoke na pendekezo la kumtaja Makamba kuwa ndiye awe mgombea urais 2015,” alisema.
Ratiba ilionyesha kuwa baada ya chakula cha mchana kulikuwa na muda wa wajumbe mmoja mmoja kutoa mawazo yake kwa mada zilizojadiliwa.
Hata hivyo, waandaaji walipoona wajumbe wanataka kuhoji jina la Makamba kutajwa ndani ya ukumbi kinyume cha mada zilivyoelekeza, walikiondoa kipengele hicho na baada ya chakula semina ilifungwa.
Lakini hadi wajumbe wanatoka ukumbini hakuna kura yoyote iliyopigwa kumpendekeza yeyote kuwa mgombea urais na wala hakuwepo mwandishi yeyote wa habari.
Viongozi hao wa vyuo wanadai kuwa Makamba amekuwa akijipenyeza katika Tahliso kwa kutumia baadhi viongozi, wakitolea mfano kongamano la Baraza la Katiba la taasisi hiyo liliofanyika Mzumbe tawi la Mbeya Agosti 2 na 3, mwaka huu.
Kwamba Tahliso baada ya kongamano walitakiwa watoe mapendekezo yao kuhusu rasimu ya katiba mpya, lakini Makamba anadaiwa kufika mkoani humo usiku na kukutana na baadhi ya wajumbe.
Katika mazungumzo na wapambe wake, inaelezwa kuwa alitaka wapenyeze suala la umri wa mgombea urais katika tamko la mapendekezo yao kwamba miaka iwe kuanzia kati ya 30 na 35 ili kumpa yeye nafasi ya kutimiza azma yake.
Mkakati huo unadaiwa kuratibiwa na kijana mmoja anayetajwa kwa jina la Tibaigana ambaye alihudhuria kongamano la Mbeya na semina ya Morogoro akijitambulisha kama mkurugenzi wa FDIP.
Katika semina ya Morogoro wajumbe walilipwa nauli kati ya sh 14,000 hadi sh 100,000 kwa kwenda na kurudi walikotoka pamoja na posho ya chakula na malazi sh 70,000 kila mmoja.

Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment